Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, akipanda mti wa kumbukumbu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Wilaya ya Karagwe wakati alipofika Chuoni hapo kushuhudia makabidhiano ya Chuo hicho kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwenda VETA.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, akikagua majengo yanayojengwa na kukarabatiwa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Wilaya ya Karagwe
Muonekano wa baadhi ya majengo yanayoendelea kujengwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi ha Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Godwin Kitonka wakisaini mkataba wa makabidhiano ya Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Halmashauri kwenda VETAWaziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, akionyeshwa baadhi ya majengo yanayojengwa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Wilaya ya Karagwe wakati alipofika Chuoni hapo kushuhudia makabidhiano ya Chuo hicho kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwenda VETA.
********************************************
Serikali imejenga na kukamilisha jumla ya Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi 41 huku vingine 29 vikiendelea kujengwa nchini, kwa lengo la kufanikisha mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda na kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako katika halfa ya makabidhiano ya usimamizi na uendeshaji wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Wilaya ya Karagwe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwenda Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika chuoni hapo mkoani Kagera.
Profesa Ndalichako amesema nia ya ujenzi wa vyuo hivyo ni kuhakikisha nchi inazalisha raslimiali watu ya kutosha yenye ujuzi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya viwanda. Katika kutimiza azma hiyo Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo vya mikoa na wilaya kwa awamu.
“Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali ilitenga shilingi bilioni 40 kwa ajili ya kujenga vyuo vipya vya VETA vya Wilaya katika Wilaya 25 za Tanzania Bara, ujenzi wa vyuo hivi unatarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa fedha na kuongeza wigo wa kuzalisha raslimali watu yenye ujuzi mahsusi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na kukuza uchumi wa Taifa letu kwa ujumla,” amesisitiza Profesa Ndalichako
Aidha, Waziri Ndalichako amewataka wananchi kutambua umuhimu wa mafunzo ya Ufundi Stadi na kuwahamasisha vijana kujiunga na mafunzo hayo ili waweze kujipatia ajira kwa urahisi na kujikwamua kiuchumi lakini pia kuchangia juhudi za serikali kwa kuchangia pato la Taifa kwa kulipa kodi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Wallece Mashanda ameishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha Shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kukarabati na kujenga baadhi ya majengo katika chuo hicho na kukubali ombi la Halmashauri ya Karagwe la kukabidhi usimamizi na uendeshaji wa chuo hicho kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
Mashanda amesema Halmashauri hiyo imeamua kukikabidhi chuo hicho kwa VETA kutokana na kutokuwa na uwezo wa kukisimamia na kukiendesha na kukosa rasilimali kwani lengo ni kuona chuo hicho kinatoa mafunzo kwa ufanisi zaidi .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Dkt. Pancras Bujulu amesema baada ya kukipokea chuo hicho shughuli za Ukarabati wa Majengo yaliyokuwepo awali na Ujenzi wa majengo mapya ya nyongeza unaendelea ambapo majengo yanayokarabatiwa ni pamoja na karakana ya Uchomeleaji na Uungaji Vyuma, karakana ya Ubunifu wa Mavazi Ushonaji na Teknolojia ya Nguo, karakana ya Ufundi Magari, karakana ya Ufungaji na Utandazaji wa Bomba na kubadili Jengo la Utawala kuwa Darasa.
Akizungumzia ujenzi wa majengo mapya katika chuo hicho Dkt. Bujulu amesema majengo yanayojengwa ni pamoja na jengo la Utawala, likiwa na Maabara ya Kompyuta, Maktaba, Karakana ya Elektroniki, na Karakana ya Umeme, bwalo la Chakula na Jiko, hosteli ya Wavulana, jengo la wazi la Mafunzo mbalimbali na la Vyoo, jengo la vyoo katika hosteli ya wasichana na stoo ya vifaa vya kufundishia