Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe.
Ummy Nderiananga akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Watu wenye
Ulemavu wakati wa kikao kazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam
Disemba 31, 2020 katika ukumbi wa Mkutano uliopo kwenye ofisi ya
halmashauri ya Temeke lengo ikiwa ni kujadiliana na kushauriana namna
bora ya kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu pamoja na kutatua
changamoto zinazo wakabili. (Kulia) ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Temeke Bw. Lusubilo Mwakabibi.
Baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu walioshiriki kikao
kazi hicho wakifuatilia kwa makini hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga
(hayupo pichani).
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Godwin Gondwe akieleza jambo wakati wa
kikao kazi cha Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alipokutana na Viongozi wa Vyama
vya Watu wenye Ulemavu kujadiliana pamoja na kushauriana namna bora ya
kuhudumia watu wenye ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazo
wakabili wenye ulemavu. (Kulia) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke Bw. Lusubilo Mwakabibi akieleza
jambo wakati wa kikao kazi hicho kilichokuwa kikiongozwa na Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy
Nderiananga wakati wa kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam
Disemba 30, 2020 katika ukumbi wa Mkutano wa uliopo halmashauri ya
Temeke. (Kushoto) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga.
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe.
Ummy
Nderiananga amewatanga Viongozi wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu
kuhakikisha wanashirikiana na Serikali ili waweze kuimarisha ustawi na
kuchochea gurudumu la maendeleo ya kundi hilo maalum.
Rai hiyo ameitoa wakati alipokutana na Viongozi wa Vyama Vya Watu
Wenye Ulemavu Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano uliopo
kwenye ofisi ya halmashauri ya Temeke lengo ikiwa ni kujadiliana
pamoja na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye ulemavu
sambamba na kutatua changamoto zinazo wakabili wenye ulemavu nchini.
Mheshimiwa Ummy alieleza kuwa Serikali inawajali na kuthamini wenye
ulemavu na katika kulitambua hilo Serikali imekuwa ikishirikiana na
asasi za Watu wenye ulemavu kwa nia njema na dhamira ya dhati ili
kutetea maslahi ya kundi hilo katika jamii inayowazunguka.
“Mkiwa
kama viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu mtambue mnajukumu na ni
wajibu wenu kushughulikia masuala mbalimbali ya wenye ulemavu kwa
kushirikiana na serikali ili kufanikisha malengo mliyonayo,”
alisema Ummy.
“Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitatua matatizo ya wananchi
papo kwa papo na ndivyo tulivyoelekezwa sisi watendaji wake kutatua
changamoto za wananchi na ndio maana nipo hapa kusikiliza kero zenu na
kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Naibu Waziri Ummy.
Alieleza kuwa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu wanatakiwa
kutambua majukumu yao na wayatekeleze kwa weledi na ufanisi ili waweze
kufanikisha masuala mbalimbali yanayowakabili wenye ulemavu.
Aliongeza
kuwa Watu wenye Ulemavu wanauwezo wa kufanya miradi mikubwa ambayo
itawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuweza kuajiri wenzao wengine wenye
ulemavu, hivyo aliwaasa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu nchini
kuanzisha miradi mikubwa.
Sambamba na hayo Naibu Waziri, amewata Maafisa Ustawi wa Jamii
kuongeza juhudi na kasi katika kuhamasisha Watu wenye Ulemavu
wananufaika na fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri ya 2% ili
waweze kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Naibu Waziri Ummy ametaka uwepo wa utaratibu mzuri na ambao
utakuwa rafiki kwa Watu Wenye Ulemavu kupata mikopo hiyo inayotolewa
na halmashauri pasipo kuwa na vikwazo vyovyote.
“Watu wenye Ulemavu wanapokuja kuomba mikopo hiyo uwepo utaratibu
ambao utaharakisha upatikanaji wa mikopo hiyo kwa kuwa kundi hili
linahitaji uangalizi maalum tofauti na mikopo iniayotolewa kwa wale
wasio na ulemavu,” alieleza Mheshimiwa Ummy
Pia, Mheshimiwa Ummy alitumia fursa hiyo kuvitaka vikundi vya watu
wenye ulemavu kuachana na kasumba kuwa mikopo wanayopatiwa na
halmashauri ya 2% kuwa ni misaada au inatolewa bure badala yake wakope
na kurejesha kwa wakati ili waweze kukopeshwa tena zaidi.
Naibu Waziri Ummy alitumia fursa hiyo kupongeza halmasuari ya Temeke
kwa namna ambavyo imekuwa ikiratibu vizuri utoaji wa mikopo ya 4% kwa
Wanawake, 4% kwa Vijana na 2% kwa Watu wenye Ulemavu.
Akizungumza kabla, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Godwin Gondwe
alieleza kuwa halmashauri ya temeke imekuwa ikishughulikia masuala ya
watu wenye ulemavu kupitia dawati la “One Stop Jawabu” na halmashauri
hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya asilimia 10 (4% Wanawake, 4% Vijana na
2% Watuwenye Ulemavu) kwa ajili ya kuwainua kiuchumi.
“Utaratibu
huu ambao tumekuwa tukiutumia Wilaya ya Temeke umehamasisha wilaya
nyingine kuja kujifunza hapa kwetu njia bora tunazozitumia katika
kuwanufaisha wananchi kiuchumi na kutatua changamoto zinazowakabili,”
alisema Gondwe
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke Bw. Lusubilo
Mwakabibi alisema kuwa Halmashauri ya Temeke imepokea maelekezo ya
Mheshimiwa Naibu Waziri na wataendelea kutatua changamoto mbalimbali
zinazolikabili kundi la wenye Ulemavu.