Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga (kushoto) akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Felix Staki wakati alipowasili chuo cha VETA Rufiji kukagua mradi wa ujenzi wa chuo hicho.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga (katikati) akipokea maelezo ya ujenzi kutoka kwa Msimamizi wa ujenzi, Erasto Thomas wakati alipowasili chuo cha VETA Rufiji kukagua mradi wa ujenzi wa chuo hicho.
Muonekano wa moja kati ya majengo yanayojengwa katika chuo cha VETA Rufiji mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga (Mb) akipitia baadhi ya nyaraka wakati alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA Rufiji.
……………………………………………………………………………..
Ukiukwaji wa taratibu katika kutunuku zabuni za upatikanaji mafundi jamii wa ujenzi wa chuo cha VETA Rufiji umepelekea kusimamishwa kazi kwa watumishi nane wa chuo cha VETA Pwani ambao walikuwa katika Kamati ya ujenzi wa chuo hicho.
Hatua hiyo imefikiwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa chuo hicho leo ambapo aligundua kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa kutunuku mafundi ujenzi kupitia force akaunti uliopelekea ujenzi wa chuo hicho kuzorota.
“Kuanzia leo nawasimamisha kazi wote waliokuwa kwenye Kamati ya ujenzi na nawaagiza Takukuru kuwafanyia uchunguzi ili kubaini kilichofanya wakakiuka utaratibu kwa kiwango kikubwa hivi,” amesema mhe. Kipanga.
Kamati hiyo ya ujenzi yenye jumla ya watu nane ilimtunuku fundi jamii mmoja aliyejulikana kwa jina la Phillipo Urasi, zabuni ya kujenga majengo 16 kinyume na utaratibu unaotaka fundi mmoja kupewa zabuni ya kujenga jengo moja tu.
Aidha, mhe. Kipanga amemsitisha fundi huyo kuendelea na ujenzi na kuagiza wachaguliwe mafundi wengine mara moja kutoka kwenye orodha ya wazabuni waliotuma maombi awali ili kazi iweze kumalizika kwa wakati.
“Naagiza pia huyo fundi Urasi asimame kazi kuanzia leo na nataka Mkurugenzi wa VETA Makao Makuu usimamie kuhakikisha wanapatikana mafundi wengine haraka, kutoka kwenye orodha ya mafundi walioomba kazi mwanzo ili kazi iendelee na kukamilika kwa wakati uliopangwa,” amesisitiza Mhe. Kipanga.
Akisoma taarifa ya ujenzi, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Pwani, Clara Kibodya amesema kuwa mpaka sasa wameshapokea jumla ya Sh. Bilioni 1.1 na kwamba ujenzi mpaka sasa umefikia asilimia 33 na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi Machi mwaka huu.
Waliosimamishwa kazi ni Leonard Mwandumbya
Mwalimu wa Umeme,
Aibu Issa Mwalimu wa Maabara, Haji Sinani Mwalimu wa majokofu na viyoyozi, David Thobias Mwalimu wa Magari, Erasto Thomas Mwalimu wa useremala na msimamizi wa ujenzi, Tumaini Magina Mwalimu wa Electronics, Paul Kimaro Mwalimu wa Engineering Science na Kubri Mkwanda Afisa Manunuzi.