IPO HAJA YA KUZIJENGEA UWEZO HALMASHAURI ZOTE NCHINI-WAZIRI UMMY

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akiwasilisha taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine na Mwenyekiti wa Bodi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Prof. Esnat Chaggu.

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine akifafanua jambo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira hii leo Jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu.

Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakifuatilia mawasilisho ya taarifa ya Muundo na Majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

…………………………………………………………………………………..

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu amesema ipo haja ya kuzijengea uwezo halmashauri zote nchini ili ziweze kuwa na usimamizi mzuri wa taka katika madampo.

Ummy amesema hayo leo Januari 27, 2020 wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu muundo wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.

Alisema kuwa kumekuwepo na changamoto ya kutokuwepo na usimamizi mzuri wa taka zinazotupwa katika madampo na badala yake zinaachwa na kurudi kwenye makazi ya watu hali inayohatarisha afya zao.

 

‘’Halmashauri zikifanya sorting (kutenganisha) aina za taka kwa mfano chupa za plastiki zinapelekwa viwandani kurejelezwa, taka za mabaki ya chakula zinafanya kuwa mbolea tutakuwa tumefanikiwa kusimamia na kudhibiti taka kwenye madampo,” alisema Ummy.

Alitaja mikakati itakayokelezwa kuwa ni pamoja na kuhamasisha usimamizi na udhibiti wa taka kwa kutumia dhana ya Punguza, Tumia tena na Rejeleza kwa lengo kupunguza gharama za usimamizi na udhibiti wa taka katika mamlaka za Serikali za Mitaa.

Pia waziri huyo alisema Serikali itaimarisha usimamizi na hifadhi ya mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu pamoja na uratibu na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira.

Kwa upande mwingine Waziri Umya alibanisha kuwa upo utegemezi mkubwa wa matumizi ya mkaa na kuni kama chanzo cha nishati ya kupikia pamoja na shughuli za kilimo zisizo endelevu jail inayosababisha ongezeko la uharibifu wa mazingira nchini.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhamasisha kampeni ya upandaji miti, matumizi ya nishati mbadala kama gesi na kuweka mikakati ya uhamasishaji wa kilimo kinachozingatia uhifadhi wa mazingira.

Aliongeza kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kupikia katika ngazi ya kaya na taasisi za umma na binafsi hususan taasisi za elimu na mafunzo, Magereza, na Majeshi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. David Kihenzile alipongeza kampeni ya Serikali kupitia Ofisi hiyo ya kupanda na miti ambapo alishauri kuwe na mikakati ya kuwa na takwimu za miti inayostawi.

Pia Kihenzile alipendekeza kuwepo na mkakati wa kujenga madampo ya kisasa katika wilaya zote ili kuweza kudhibiti taka na kuyafanya maeneo hayo kuwa masafi.

‘’Ningependekeza tuwe na mikakati kabambe ya kupanda miti na tunaweza kuwa na mkakati maalumu kwa Jiji hili la Dodoma ambalo kwa sasa ndio makao makuu ya nchi,” alishauri Kihenzile. 

Post a Comment

Previous Post Next Post