AWESO AMUAGIZA DC RORYA KUMSAKA MKANDARASI ALIYETEKELEZA MRADI WA MAJI KIROGO

 

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akikagua ujenzi wa tenki la mradi wa maji wa Komuge wilayani Rorya

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisikiliza maelezo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Komuge, wilayani Rorya.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akikagua utekelezwaji wa chanzo cha maji cha mradi wa Komuge, wilayani Rorya. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari ChegeWaziri wa Maji, Jumaa Aweso akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya Simon Odunga (kulia mwenye miwani) mara baada ya kutembelea mradi wa maji wa Kirogo

***************************************************

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga kumtafuta mkandarasi aliyehusika na ujenzi wa mradi wa maji wa Kirogo wilayani humo.

Ametoa agizo hilo Januari 6, 2021 alipofanya ziara ya kukagua mradi na kujiridhisha kuwa mkandarasi wake alillipwa shilingi bilioni 1 ambayo ni sawa na asilimia 98 ya mkataba wake licha ya kwamba mradi huo haujakamilka.

“Mkuu wa Wilaya, ninakuelekeza kuwaita wote waliohusika na ujenzi wa mradi huu na hatua stahiki zichukuliwe haraka, hatuwezi kukubali wananchi wateseke, fedha tumelipa wakati mradi haujakamilika,” alielekeza Waziri Aweso.

Alibainisha kwamba Wilaya ya Rorya ni kichaka cha watu wachache kujinufaisha na fedha za mradi wa maji na kwamba hilo sasa limefikia kikomo.

“Kwanini mkandarasi amelipwa fedha yote yaani asilimia 98 haliyakuwa mradi haujakamilika,” alihoji Waziri Aweso

Alisema inawezekana wakandarasi waliokuwa wakipewa kazi za ujenzi wa miradi wilayani humo hawakuangaliwa uwezo wao wa utekelezaji wa miradi na badala yake wamekuwa wakipewa kazi kiujamaa na alitahadharisha kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kupeana kazi kwa namna hiyo.

“Kama kuna mhandisi wa maji ambaye amethibitisha pesa mtu huyu kulipwa na yeye ni mtaalam ambaye analipwa mshahara na yupo kwa ajili ya kusimamia wananchi wapate huduma ya maji kwa niaba ya Wizara lakini amefanya mchezo ili kumnufaisha mkandarasi wakati wananchi wanateseka hata kama amehamishwa huko alipo tutamchukulia hatua,” alisisitiza Waziri Aweso

Waziri Aweso alikagua mradi huo wenye vituo 27 vya kuchotea maji kwa ajili ya vijiji vya Kirogo, Wamaya na Nyabiwe na kukuta vituo vichache vikifanya kazi na huku vingi vikiwa havitoi maji bila kuwepo sababu ya msingi wala maelezo yanayojitosheleza jambo ambalo lilimkera.

Alimuelekeza Mkuu wa Wilaya kumuita Mhandisi wa maji aliyesimamia ujenzi wa mradi huo afike hapo mara moja ili uchunguzi ufanyike haraka.

“Apigiwe simu aje kesho aeleze ni kwanini mradi umekabidhiwa kwa wananchi hali yakuwa haujakamilika na waliohusika kufanya ubadhirifu hii tabu wanayopata wananchi sasa hivi na wao hao waipate, yeyote atakayebainika amekula fedha za miradi ya maji ajiandae kuzitapika mchana kweupe,” alisisitiza Waziri Aweso.

Waziri Aweso aliwataka wataalam kwenye Sekta ya Maji kuacha mara moja tabia ya kuwajengea wananchi chuki kwa Serikali yao “wataalam kwanini mnakua waongo, mnajenga chuki kwa serikali, inakuaje upokee mradi ambao haujakamilika, unapewa fedha za kukagua miradi lakini hufanyi hivyo,” alihoji Waziri Aweso.

Alielekeza wasimamizi wa miradi ya maji kote nchini (wilayani na mikoani) kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa Serikali kwenye maeneo yao na pia wahakikishe wanawasilisha taarifa za miradi kwenye vyombo vya maamuzi ikiwemo baraza la madiwani juu ya shughuli wanazoendelea nazo na alisisitiza kwamba mhandisi atakeyekaidi wizara itamchukulia hatua. 

Aidha, ameelekeza Wiki ya Maji mwezi Machi iwe ni maalum kwa jili ya uzinduzi wa miradi. “Tarehe 22 Machi, Wiki ya maji hatutaki iwe ya porojo na mapambio, tunataka iwe ya uzinduzi wa miradi, tunataka wiki ya maji iwe ni ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kutoa zawadi ya miradi ya maji kwa wananchi wake,” alielekeza Waziri Aweso.

Mara baada ya ziara za ukaguzi wa miradi, Waziri Aweso atakutana na watumishi wote wa Sekta ya Maji Mkoani Mara kujadili changamoto zinazokwamisha shughuli za kuwafikishia wananchi huduma ya maji ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja

Post a Comment

Previous Post Next Post