ZAIDI YA WAKULIMA NA WAFANYABIASHARA 200 WAPATIWA MAFUNZO YA UZALISHAJI NA USINDIKAJI MAFUTA YA KULA MKOANI KIGOMA

 

********************************

Zaidi ya wakulima na wafanyabiashara wa mafuta ya kula 220 Mkoani Kigoma wamepatiwa mafunzo ya uzalishaji na usindikaji wa mafuta kwa kuzingatia matakwa ya Viwango na vifungashio bora ili kuongeza thamani ya mafuta hayo.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo katika ukumbi wa Chuo cha waganga Kigoma mjini, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. Lazaro Msasalaga alisema ili mafuta ya kula yawe bora ni lazima kuzingatia kanuni bora za kilimo, usindikaji na afya.

Bw. Msasalaga alisema wazalishaji wengi wa mawese na mafuta mengine ya kula wamekua wanatumia njia za asili ambazo hazizingatii ubora na usalama wa mafuta hayo na hivyo kusababisha madhara kwa walaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa TBS Bw. Rodney Alananga aliwataka wasindikaji kufuata taratibu za uthibitishaji ubora wa mafuta hayo kwani kwa kufanya hivyo kutaongeza masoko ya ndani na nje ya nchi na vilevile kutalinda afya na usalama wa walaji.

Wakati huo huo Meneja Mafunzo na Utafiti wa TBS , Bw Hamis Sudi akifunga mafunzo hayo katika kata ya Ngaruka wilayani Katavi alisema serikali inathamini mchango wa wajasiriamali katika kukuza uc humi wa nchi, hivyo itaendelea kutoa mafunzo haya nchi nzima lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wazalishaji wa mafuta ya kula nchini wanazalisha bidhaa hiyo kwa kuzingatia viwango vya kitaifa vilivyopo.

Bw. Sudi alisema mbali na mafunzo haya TBS imekuwa ikitoa huduma za kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali bure kwa miaka mitatu ya kwanza lengo likiwa ni lilelile la kuwawezesha wajasiriamali ili waweze kukuwa na kuzalisha bidhaa bora ambazo zitashindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Ninawasihi wajasiriamali mtumie fursa hii muhimu ambayo serikali imewapatia ili muweze kuinua kipato chenu binafsi na taifa kwa ujumla”, alisisitiza Bw. Sudi.

Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Festo Kapela alieleza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya mafuta ya kula yanayotumika nchini hutoka nje ya nchi kwa kutumia gharama kubwa na kwamba ikiwa mafuta ya mawese yatapewa ubora Serikali itaokoa gharama kubwa.

“Nchi za Afrika Mashariki na kati zinategemea sana mafuta ya nje na nchi ambapo kama viwanda vya kuchakata mafuta ya mawese na kuongezwa ubora itakua fursa kwa wakulima na wasindikaji kuongeza pato la Taifa kupitia soko la mafuta”, alisema Kapela.

Mafunzo haya yaliyohusisha vituo 15 mkoani Kigoma ni mwendelezo wa mafunzo yaliyoanza kutolewa mapema mwezi Agosti mwaka huu, yakianzia kanda ya kati, na sasa kanda ya Magharibi itakayofikia pia mikoa ya Katavi na Rukwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post