WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, DKT.NDUMBARO AWATAKA WAKAZI WA MKOA WA LINDI KUCHANGAMKIA FURSA ZA UTALII

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumaro akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Maj.Gen.( Mst) Hamis Semfuko wakipata maelezo kuhusiana na msikiti mkubwa wa kale kutoka kwa Mercy Mbogelah Meneja Mhifadhi Malikale katika Urithi wa utamaduni wa dunia magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( kushoto) akiwa pamoja na Mwenyekii wa Bodi ya TAWA, Maj.Gen.( Mst) Hamis Semfuko wakipatiwa maelezo kuhusiana na magofu ya kale kutoka kwa Mercy Mbogelah Meneja Mhifadhi malikale katika Urithi wa utamaduni wa dunia magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo mnara

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro( wa kwanza kulia) akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Maj.Gen.( Mst) Hamis Semfuko wakifurahia jambo wakiwa kwenye boti inayomilikiwa na TAWA ikiwa inaelekea katika Hifadhi ya urithi wa utamaduni wa Dunia Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

**************************************

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amewataka Wakazi wa Mkoa wa Lindi kuchangamkia fursa za utalii zilizopo katika mkoa huo.

Ameyasema hayo leo wakati alipotembelela Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni  wa Dunia, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songomnara ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli.

Amesema kazi ya Serikali sio kutoa fedha kwa mtu mmoja mmoja bali kuweka mazingira mazuri na kutengeneza fursa kwa wananchi waweze kuendesha shughuli za kiuchumi kwenye maeneo hisika.

Amesema mkoa wa Lindi hasa wilaya ya Kilwa umejaliwa kuwa na aina lukuki za vivutio vya Utalii  ikiwemo vivutio vya utalii vya mambokale, uwindaji wa kitalii, utalii wa fukwe pamoja na  utalii wa picha.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Lindi unashika nafasi ya pili katika mikoa yenye maeneo ya misitu mikubwa nchini ikiongozwa na mkoa wa Katavi ambao una asilimia 82.7 ya eneo lake limefunikwa na misitu.

” Nimeamua kuanza ziara yangu  katika mkoa huu ili kuja  kuwambia   Wana Kilwa mmekaa juu ya dhahabu changamkeni ‘” amesisitiza Ndumbaro.

Akizungumza na Wakazi hao wa Kilwa Kisiwani, Dkt. Ndumbaro amewataka Wananchi hao kichangamkia fursa  hizo  zinazoambatana na utalii kama vile chakula,  usafiri, huduma za malazi pamoja na ngoma za asili baadala ya kuwa Walalamikaji.

” Shida tuliyo nayo sisi tunapenda vitu virahisi rahisi na tumekuwa sio watu wa kupambana na tumekuwa tukichukua muda mwingi kuilaumu Serikali badala ya kuzitumia fursa hizi. Alisisitiza Dkt.Ndumbaro.

Amewataka Wananchi hao kubadilika na kuanza kuchangamkia  fursa nyingi zilizopo ili waweze kuwa matajiri.

” Wizara ya Maliasili na Utalii tumewaletea Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) ili kuboresha maeneo ya vivutio vya utalii vya Mambokale  ili wananchi mpate na serikali ipate pia ” amesisitiza Dkt.Ndumbaro.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA,  Maj.Gen ( Mst), Hamisi  Semfuko amewataka wakazi hao kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuviendeleza vivutio vya kihistoria vya utalii ili viweze kuwasaidia kiuchumi.

Amesema moja ya hatua ambazo TAWA wamezichukia katika magofu hayo  ni kununua boti mpya ya kisasa kwa ajili ya usafiri kwa watalii pamoja na kuweka miundombinu wezeshi kwa ajili ya watalii kutembelea eneo hilo.

Awali Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilwa Kisiwani, Shabani Ali ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TAWA kwa kuyakarabati magofu hayo ambayo yalikuwa kwenye hali mbaya

” Kwa sasa tumeanza kuona matunda ya magofu haya Watalii  wamekuwa wakitembelea kwa wingi katika maeneo haya tofauti na kipindi cha nyuma kabla ya ujio wa TAWA.

Post a Comment

Previous Post Next Post