DKT CHAULA ARATIBU MKAKATI WA KUIPELEKA JAMII YA TANZANIA KIDIJITALI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akiongoza kikao cha kamati ya kujadili na kupitisha mpango mkakati wa kuipeleka jamii ya Tanzania katika mfumo wa kidijitali, katika ukumbi wa Wizara hiyo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza katika kikao cha kamati ya kujadili na kupitisha mpango mkakati wa kuipeleka jamii ya Tanzania katika mfumo wa kidijitali, katika ukumbi wa Wizara hiyo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula.

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi (Kulia) wakiteta jambo katika kikao cha kamati ya kujadili na kupitisha mpango mkakati wa kuipeleka jamii ya Tanzania katika mfumo wa kidijitali, katika ukumbi wa Wizara hiyo, Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), Waziri Kindamba na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba wakizungumza jambo katika kikao cha kamati ya kujadili na kupitisha mpango mkakati wa kuipeleka jamii ya Tanzania katika mfumo wa dijitali, katika ukumbi wa Wizara hiyo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma

Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mulembwa Munaku (aliyesimama) akiwasilisha Mkakati wa Kuipeleka jamii ya Tanzania kidijitali kwa wajumbe wa kamati ya mkakati huo katika ukumbi wa Wizara hiyo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma

***************************************

Prisca Ulomi na Faraja Mpina, WMTH

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WMTH), Dkt. Zainab Chaula ameratibu mpango mkakati wa pamoja wa kuipeleka jamii ya kitanzania katika mfumo wa dijitali kwa kuanza na Sekta ya Elimu na Sekta ya Afya ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja.

Dkt Chaula ameendesha  kikao cha kamati ya utekelezaji wa mkakati huo katika ukumbi wa Wizara hiyo mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma kwa lengo la kujipanga na kuridhia mkakati huo ili kuhakikisha kunakuwa na uratibu mahsusi unaokidhi malengo yaliyokusudiwa badala ya kila Wizara, taasisi au wadau kufanya kazi peke yao bila uratibu.

Kamati hiyo inajumuisha taasisi za Serikali ina mpango wa kuwashirikisha wadau mbalimbali wanaopeleka intaneti katika shule za umma, hospitali na vituo vya afya ili kuhakikisha huduma za mawasiliano na intaneti zinazotolewa na wadau zinakidhi mahitaji na vigezo vilivyokusudiwa vya kuipeleka jamii ya kitanzania katika mfumo wa kidijitali, aliongeza Dkt. chaula

“Sisi kama Wizara tuna malengo na matamanio yetu, kupitia Sera ya TEHAMA ya Wizara ya mwaka 2016 ili kwa pamoja kama Serikali tujipange, turidhie na tushirikishe wadau wote wanaotuwezesha katika eneo hili ili kurahisisha ukusanyaji wa takwimu na kujua maeneo yaliyofikiwa”, alisisitiza Dkt. Chaula

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Serikali imejenga miundombinu mbalimbali katika Sekta ya Afya na Elimu na kuongeza idadi ya shule, hospitali, vituo vya Afya, barabara pamoja na ufikishaji wa umeme vijijini kupitia REA na kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya upelekaji wa huduma za intaneti katika maeneo hayo.

Aliongeza kuwa wananchi wanaofikiwa na hizi huduma wanatakiwa kushiriki katika uchumi wa kidijitali na Wizara ina jukumu la kuhakikisha huduma za mawasiliano na data zinawafikia

wananchi kwa kushirikiana na wadau ili juhudi za Serikali ziwe na matokeo chanya katika utoaji wa huduma bora katika Sekta ya Elimu na Afya.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa mkakati huo una lengo la kuhakikisha miundombinu ya TEHAMA na huduma za mawasiliano zinatumika katika Sekta ya Afya na Elimu na kutimiza lengo la Serikali kupitia Wizara hii iliyopewa dhamana la kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 asilimia 80 ya wananchi wamefikiwa na huduma za intaneti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Ofisi ya Rais Tawala na Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Erick Kitali amesema kuwa mkakati huo utasaidia utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kwa gharama nafuu kama vile vituo vya kutolea huduma jumuishi “one stop centr”’ na huduma za tiba mtandao ambapo mpaka sasa ni vituo 12 tu ndio vimeunganishwa na huduma hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba amesema kuwa UCSAF ina jukumu la kuhakikisha TEHAMA inaleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi na mpaka sasa wameshapeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 711, intaneti katika shule 481 pamoja na kuwezesha tiba mtandao.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia; Wizara ya Afya; TAMISEMI na wakuu wa taasisi za UCSAF; Shirika la Mawasiliano Tanzania; na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania

Post a Comment

Previous Post Next Post