WANANCHI WA KAGERA WATOA KERO ZAO ZA UMEME KWA NAIBU WAZIRI BYABATO


 TANESCO NA REA WAELEKEZWA KUTATUA CHANGAMOTO HIZO

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, amekutana na wananchi wa Mkoa wa Kagera, Uongozi na Watumishi wa TANESCO na REA, baadhi ya Watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukoba, kusikiliza kero za wananchi wa Kagera kuhusu huduma ya umeme. 

Miongoni mwa kero zilizotolewa na wananchi hao wa mkoa wa Kagera ni malalamiko ya baadhi ya wananchi kufyekewa mazao yao ikiwemo migomba na mazao mengine wakati wa kupitisha miundo mbinu ya umeme, umeme kuwa hafifu wakati wa mahitaji makubwa kuanzia saa moja jioni hadi saa tatu usiku katika baadhi ya maeneo ya Bukoba na Bunazi wilayani Misenyi, 

kuchelewa kulipwa fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi wa Kakono utakaozalisha umeme wa Mw 87 katika mto Kagera, kuchelewa kuunganishiwa umeme baada ya kulipia na baadhi ya vijiji kuwa vimerukwa kuunganishiwa umeme lakini vya mbele yake vimeunganishiwa umeme. 

Akijibu kero zilizotolewa na wananchi wa Mkoa wa Kagera, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato ameilekeza TANESCO na REA, kutatua changamoto hizo zilizotolewa na wananchi hao na kutoa maelekezo kwa TANESCO na REA kuhakikisha wateja wote 881 waliolipia kuomba kuunganishiwa huduma ya huduma ya umeme hadi tarehe 22 Mwezi Desemba, 2020, wote wawe wamepatiwa huduma hiyo, ifikapo tarehe 31 Mwezi January, 2021.

Aidha, Naibu Waziri Byabato ameilekeza TANESCO kuhakikisha kuwa, kazi zote zilizoachwa na mkandarasi wa REA 11 UR kuwa zinakamilishwa ifikapo mwezi May 2021.

Naibu Waziri Byabato, amewaelekeza TANESCO kuitumia ipasavyo ofisi ya uhusiano kwa wateja na kuhakikisha kwamba wateja wanapatiwa taarifa za hatua mbalimbali za maombi yao kuhusu kuunganishiwa umeme kwa njia ya simu au ujumbe mfupi wa maandishi .

Vilevile, Naibu Waziri huyo wa Nishati, amewaelekeza TANESCO wawajulishe wateja kama kuna matengenezo yoyote ya lazima au hitilafu zinazotokea katika miundombinu ya umeme na kuwaelekeza TANESCO kuwaunganishia umeme Wateja ndani ya siku 7 mara baada ya kulipia.

Akizungumzia kuhusu suala la fidia kwa wananchi wanaotakiwa kupisha miundo mbinu ya umeme, Naibu Waziri Byabato amewafafanulia wananchi wa mkoa wa Kagera kuwa, vitongoji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa umeme vitaunganishiwa umeme katika mpango maalum wa kuunganisha umeme wateja kwenye vitongoji vyote nchini ( Desfication)

Akijibu kuhusu mazao yaliyokatwa wakati wa kupitisha miundombinu ya umeme, Naibu Waziri Byabato, amesema, Mradi wa REA unaotekelezwa, umegharamiwa na Serikali kwa asilimia 100, hivyo hauna fidia.

Naibu Waziri Byabato amewaomba wananchi kuwa, waruhusu miundombinu hiyo ipite, ili wapatiwe huduma ya umeme.

Akijibu kuhusu fidia ya Mradi wa Kakono, Naibu Waziri Byabato, amesema Serikali imekamilisha hatua za uhakiki kwa wake wote watakaoathirika na mradi huo na kuwa, kwa sasa Wizara ya Fedha inashughulikia malipo yao.

Mkutano huo wa kusikiliza na kutatua kero za umeme wanazozipata wananchi wa mkoa wa Kagera, umefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu mkoa wa Kagera, tarehe 22 Desemba, 2020.

Post a Comment

Previous Post Next Post