Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewataka baadhi ya viongozi wa vijiji na kata wanaoshirikiana na wafugaji kuvunja sheria, taratibu na kanuni za nchi ili kuwanyanyasa wakulima katika maeneo yao kuacha mara moja kufanya hivyo kwani viongozi hao wanakuwa wanashiriki katika migogoro kwa kuchonganisha wakulima na wafugaji.
Akizungumza jana (22.12.2020) wilayani Liwale, kwenye kikao kilichoshirikisha wakulima na wafugaji wa Mkoa wa Lindi kwa ajili ya kutatua kero zao, Waziri Ndaki amekemea urafiki wa baadhi ya viongozi hao na wafugaji ambao umekuwa ukilenga kuwanyanyasa wakulima kutokana na wafugaji kuingiza mifugo kwenye maeneo ya wakulima hao.
“Wakati mwingine mnawapa tabu wakulima kwa sababu wafugaji wanashirikiana na hawa viongozi wetu wa ngazi za chini kufanya mambo yasiyotakiwa sasa tuache, watendaji wa vijiji na kata fuateni sheria, taratibu na kanuni mlizoelekezwa zinazopaswa kuwaelekeza katika kutenda kazi zenu.” Amesema Mhe. Ndaki
Aidha, Waziri Ndaki amefafanua kuwa siku zote wakulima na wafugaji zimekuwa ni jamii zinazoelewana kwa sababu kila mmoja amekuwa akihitaji huduma kutoka kwa mwenzake, kwa maana ya mazao ya kilimo na mifugo na kutaka uhusiano huo usiharibiwe na baadhi ya viongozi wa ngazi za chini kuingia katikati yako kwa maslahi binafsi na kutaka urafiki usio na tija kwa wakulima kati ya baadhi ya viongozi hao na wafugaji ufe mara moja.
Pia, kuhusu sheria, taratibu na kanuni za nchi waziri huyo amesema nchi haiwezi kuendeshwa kwa sababu jamii moja ya watu wakali na wengine wapole bali lazima ifuate sheria, taratibu na kanuni zilizopo kutokana na wakulima kulalamikia vitendo vya baadhi ya wafugaji kuwa wakali wanapoingia katika maeneo yao na kulisha mifugo mazao ya wakulima.
“Tukifuata sheria itatusaidia sana kuishi pamoja kama nchi wakulima na wafugaji fuateni sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili tuishi pamoja, na sheria zimewekwa na wawakilishi wenu wabunge kwamba wananchi tukiwawekea utaratibu wa namna hii tunaweza kuishi kwa amani na utaratibu.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameuarifu mkutano huo wa Mkoa wa Lindi kati ya wakulima na wafugaji kuwa ni muhimu wafugaji kushirikiana na serikali katika kujenga miundombinu ya ufugaji yakiwemo malambo ya kunyweshea mifugo yao maji kwenye maeneo ambayo wamekabidhiwa na serikali kufuga mifugo kwa kuwa mahitaji ya wafugaji ni mengi na hayawezi kukamilishwa na serikali pekee kwa mara moja.
“Mahitaji ya wafugaji ni mengi wanahitaji malambo, malisho, majosho na minada haya yote kwa mara moja inawezekana kabisa serikali isiweze kufanya kwa mara moja, ombi langu kwa wafugaji ninaomba tushikiriane sisi wizara tunaweza kutengeneza michoro ya aina ya malambo yanayotakiwa kuwepo ikiwemo gharama, lakini pia tunaweza kupata pesa kiasi sasa naomba tushirikiane, wizara tukipata pesa kidogo tutawachangia nanyi mtafute pesa kupitia umoja wenu ili tugharamie kwa pamoja hayo malambo kwa kufanya hivyo itawezekana kabisa lakini mkubali nyinyi ni matajiri.” Amesema Mhe. Ndaki
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaangalia kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 kutenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kujengea malambo katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuanzia na baadhi ya vijiji kwa kushirikiana na halmashauri.
Akizungumza kwenye kikao hicho kuhusu ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Ngongo yaliyopo halmashauri ya Manispaa ya Lindi, ambayo ameyatembelea siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi Mkoani Lindi (21.12.2020) na kushuhudia kukamilika kwa ujenzi wa jengo la machinjio hayo, ambapo inasubiri awamu ya pili ya ujenzi ya kuweka vifaa vya kuchinjia na kuchakata nyama, Waziri Ndaki amesema ataongea na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, kuingiza bajeti ya awamu ya pili ya ujenzi huo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 badala ya 2022/2023 ambapo ujenzi huo umewekwa sasa unaokadiriwa kugharimu Shilingi Bilioni 2.5.
Waziri Ndaki amesema kwa kuwa jengo la machinjio limekamilika ni vyema likamilike kwa kuwekewa vifaa mapema ili machinjio hayo yaanze kufanya kazi na kuwanufaisha wafugaji kwa kuwa kwa sasa mikoa ya Kusini ukiwemo Mkoa wa Lindi na Mtwara imeanza kupokea mifugo mingi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, hivyo hitaji la mazao ya mifugo litaongezeka na mkoa utaongeza mapato kupitia machinjio hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi amesema mkoa umeweka utaratibu wa kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ambao wamekuwa wakiingia katika mkoa huo, lakini wanakabiliana na gharama kubwa katika upimaji wa maeneo hali iliyolazimu mkoa kusitisha kupokea mifugo kwa sasa kwa kuwa maeneo yaliyotengwa ni machache.
“Tunaomba wizara ione namna gani na TAMISEMI tunaweza kuja na mpango wa kuziwezesha halmashauri ili ziweze kupima maeneo kwa kasi ambayo inaweza kusaidia kutosheleza mifugo kwa sasa hivi niseme mheshimiwa waziri na ukweli kabisa tumesema tusipokee tena mifugo kwa sababu hatuna pakuiweka, ardhi tunayo lakini hatuna sehemu tulizopima hivyo mifugo ikija inakuwa vurugu na kukaribisha ugomvi kati ya wafugaji na wakulima.” Amefafanua Mhe. Zambi
Mhe. Zambi pia amesema ni muhimu kuangalia namna ya kudhibiti idadi ya mifugo kutokana na wafugaji kuwa na mifugo mingi huku wakiendelea kuishi maisha duni na kutaka kuwepo na sheria ya kudhibiti idadi ya mifugo.
Pia amekemea matumizi ya silaha ya baadhi ya wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima hali ambayo inatishia usalama wa wananchi wenzao na kuharibu mazao ya wakulima.
Nao baadhi ya wakulima na wafugaji waliozungumza katika kikao hicho wamepongeza jitihada za Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Mkoa wa Lindi kwa kuwepo kwa mkutano huo kati ya wakulima na wafugaji wenye lengo la kusikiliza kero zao na kuangalia namna ya kuzitatua.
Wametaka wakulima na wafugaji ambao watakiuka sheria, taratibu na kanuni zilizopo kwenye maeneo yao juu ya maeneo ya wafugaji na wakulima wachukuliwe hatua za kisheria badala ya kuadhibu kundi lote la jamii ya mtu mmoja aliyeshindwa kufuata sheria, taratibu na kanuni.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Lindi ukiwa ni mkoa wake wa kwanza nje ya Dodoma kufanya ziara mara baada ya kushika wadhifa huo, akisaidiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akipatiwa taarifa ya Mkoa wa Lindi na mkuu wa mkoa huo Mhe. Godfrey Zambi wakati Waziri Ndaki alipofika katika Wilaya ya Liwale kabla ya kuhudhuria mkutano kati ya wakulima na wafugaji ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Mkoani Lindi.
Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji wa Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Rogers Shegoto akielezea umuhimu wa kuendeleza maeneo ya malisho kwa kupanda malisho ya mifugo pamoja na kujenga miundombinu ya maji ili kudhibiti migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, wakati wa kikao cha wakulima na wafugaji Mkoa wa Lindi kilichofanyika wilayani Liwale.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi akizungumza kwenye kikao kati ya wakulima na wafugaji wa mkoa huo kilichofanyika wilayani Liwale kwa ajili ya kutatua kero zao na kusema kuwa mkoa unakabiliwa na gharama kubwa ya kupima maeneo ya wafugaji hali iliyowalazimu kusitisha kupokea mifugo kwa sasa kutoka nje ya mkoa huo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza kwenye kikao kati ya wakulima na wafugaji Mkoa wa Lindi kilichofanyika wilayani Liwale na kuwataka viongozi wa ngazi za chini kutokuwa chanzo cha migogoro kati ya jamii hizo mbil