TBS YAENDELEA KUTOA ELIMU YA USINDIKAJI NA UHIFADHI BORA WA MAFUTA YA KULA

 

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS Bw. Lazaro Msasalaga, akitoa elimu kwa wadau wa mafuta waliokusanyika katika ukumbi wa KAHAM wilayani Kakonko mapema wiki hii.

Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa TBS Bw. Rodney Alananga, akitoa elimu ya uhifadhi na ufungashaji bora wa mafuta ya kula kwa wauzaji wa mafuta hayo katika soko wilayani Kibondo.

************************************

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa mafuta ya kula nchini katika Wilaya za Mkoa wa Kigoma kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya umuhimu wa kuzalisha bidhaa bora na uhifadhi bora wa bidhaa hiyo ambapo mpaka sasa tayari Wilaya za Kigoma Mjini, Kakonko, Kibondo na Kasulu zimeshafikiwa.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa TBS Bw. Lazaro Msasalaga, alisema kuwa ili mafuta yakidhi viwango ni lazima kufuata kanuni bora za kilimo ikiwemo kutumia mbegu bora na kuvuna kwa wakati, kanuni bora za usindikaji na kanuni bora za usafi ikiwemo uhifadhi wa mafuta ya kula katika eneo ambalo halipigwi na jua kwani kwa kufanya kinyume na hivyo itasababisha kuzalishwa kwa kemikali zisizofaaa kwa binadamu katika mafuta hayo na kusababisha madhara makubwa ikiwemo magonjwa.

Bw. Msasalaga alisisitiza zaidi ni lazima kufuata kanuni hizo kwa pamoja na siyo kutegemea kanuni ya eneo moja tu kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha bidhaaa kutokidhi matakwa ya viwango.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa TBS Bw. Rodney Alananga, alitoa elimu kuhusu taratibu za uthibitishaji wa bidhaa na usajili wa bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi ambapo aliwaasa wenye majengo na bidhaa zote zinazotakiwa kusajiliwa wafanye hivyo haraka kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Mafunzo haya yamehusisha pia Taasisi mbalimbali ikiwemo SIDO, Wakala wa Vipimo, BRELA pamoja na Maafisa Biashara, Afya na Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri husika.

TBS tayari imekwishatoa elimu ya aina hii awamu ya kwanza katika kanda ya kati ambayo ilihusisha wilaya zilizopo mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora ambapo wadau zaidi ya 1700 walifikiwa, na kuna mpango wa kuhakikisha wilaya zote nchini zinafikiwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post