TUME YA UCHAGUZI YAMALIZA MZIZI WA FITINA

 

*************************************

Na Judith Mhina-Maelezo

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemaliza mzizi wa fitina kwa kuhakikisha vituo vyote vya uchaguzi kuna kuwa na fomu namba 14 hadi 24 zinazokidhi na kutatua changamoto mbalimbali ambazo kutokana na uzoefu uliopita zitamaliza kabisa changamoto zilizokuwa zinajitokeza.

Hayo yamebainika katika mafunzo yaliyotolewa na NEC kwa waandishi wa habari, ambapo madhumuni ya  mafunzo hayo  ni kutoa elimu kwa waandishi hao jinsi ya kutoa taarifa katika mchakato mzima wa kupiga kura tarehe 28 Oktoba 2020.

Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na waandishi hao Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka Zanzibar Hamid Mwanga amesema lengo lakutoa mafunzo hayo ni kuhakikisha wasimamizi, wasimamizi wasaidizi na mawakala wanaweza kuhudumu vema kwa kuhakikisha kila raia ambaye anastahili kupiga kura anapata nafasi hiyo bila kupata bughudha ya aina yeyote.

“Ili kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa amani,  huru na haki kama alivyoahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli Tume imekuwa na wajibu wa kufanyia kazi changamoto zote ambapo kuna fomu zinazotekeleza kutatua changamoto yeyote itakayojitokeza wakati wa kupiga kura ambazo ni  fomu namba 14 mpaka 24.

Baadhi ya changamoto ambazo zinatatuliwa katika fomu hizo ni pamoja na kuridhika au kutoridhika kwa wakala wa upigaji kura kab;a ya kuanza upigaji kura na baada ya upigaji kura, pili, malalamiko ya mpiga kura kuhusu mwenendo wa upigaji kura katika kituo eneo la upigaji kura. Aidha, fomu nyingine ni tammko la mpiga kura iwapo mpiga kura, kura yake imekataliwa kwa sababu moja au nyingine, pia, kuna fomu ya  kibali cha mtendaji wa uchaguzi na wakala wa upigaji kura kupiga kura katika kituo ambacho hakujiandikisha.

Aidha, fomu hizo zinajumuisha kibali cha mgombea kupiga kura kituo ambacho hakujiandikisha, taarifa ya msimamizi wa kituo cha kupiga kura na fomu 21 ambayo ina sehemu A, B na  C ambapo A inawakilisha matokeo ya uchaguzi wa Rais katika kituo cha kupiga kura, B matokeo ya Ubunge  na C matokeo ya Diwani. Vilevile fomu namba 22 A ni matokeo ya uchaguzi wa Rais katika kituo cha kupiga kura, B  ya Ubunge na C ya udiwani.Wakati fomu namba 23 A ni jedwali la matokeo ya uchaguzi wa Rais katika Jimbo kwa kila chama, 23 B ni ya ubunge na C ni ya Udiwani.    

Akitoa maelezo kuonesha Kifungu cha 82 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 4 ya mwaka 2018 kinasema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar-ZEC itaweka utaratibu wa upigaji kura ya mapema siku moja kabla ya siku ya upigaji kura, kifungu hicho kinaipa ZEC mamlaka ya kuratibu upigaji kura ya mapema siku moja kabla ya siku ya upigaji kura. Hivyo Sheria inaruhusu watendaji na wasimamizi wa uchaguzi Zanzibar kupiga kura tarehe 27 Oktoba siku moja kabla ya uchaguzi.

Sheria hiyo ya Zanzibar haihusiki na Sheria ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo, kwa upande wa Bara utajaza fomu namba 18 (kibali cha mtendaji wa uchaguzi na wakala wa upigaji kura kupiga kura katika kituo ambacho hakujiandikisha) inayoelekeza mtendaji yeyote yule ambaye hayupo katika kituo chake alichojiandikisha kuweza kuijaza  na kuruhusiwa kupiga kura kwenye eneo analofanyia kazi siku hiyo ya kupiga kura.

Mwanga amefafanua umuhimu wa wagombea wote wa vyama vya siasa Tanzania Bara na Visiwani wanaogombea   nafasi mbalimbali kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani huru na haki kwa kila raia wa Tanzania  aweze kuridhika na uchaguzi huo ikiwa ni pamoja  na tatizo lolote litakalojitokeza katika kituo cha kupigia kura litatuliwa mara moja ndani ya kituo husika

Akitoa mada kuhusu sheria, taratibu na miongozo iliyotolewa na  uwepo wa fomu hizo Mwanasheria wa Tume ya Uchaguzi Athumani Kimia amesema kuwa wasimamizi wa Uchaguzi na wasaidizi wao, wagombea, mawakala na waangalizi wa uchaguzi wote wamepewa elimu ya uwepo wao katika vituo vya kupigia kura hivyo kila mmoja azingatie kile kilichompeleka pale kituoni ili kulinda amani na kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani,  huru na haki.

“Tume ya Uchaguzi imehakikisha inafanyia kazi changamoto zilizowasilishwa katika Tume na kuweka utaratibu mzuri wa uwepo wa hizo  fomu ili kila raia aweze kuhudumiwa ipasavyo na kutumia haki yake ya msingi ya kupiga kura bila kubughudhiwa. Aidha, jambo la msingi kwa wale wasio na vitambulisho vya kupigia kura leseni za udereva au kitambulisho cha Taifa -NIDA kitatumika mara baada ya kupitia Daftari la Mpiga Kura lililopo katika kituo husika na kuainisha vielelezo  vya pande zote mbili ili kujiridhisha na kuweza kumruhusu mhusika kupiga kura”.

Ameongeza na amesema kuwa kwa wale ambao watakuwa wamekosea au kufanya kosa kwenye karatasi wakati wa kupiga kura, mfano ameweka tiki kwa mgombea amtakaye na kuweka mkasi kwa mgombea asiyemtaka na kugundua kuwa amefanya kosa atatoa hoja yake kwa wasimamizi wa uchaguzi ili  apewe  nafasi nyingine ya kupiga kura na kuhakikisha harudii makosa aliyoyafanya awali. Hii ina maana alama yeyote utakayoiweka kwa maana ya tiki au mkasi zote ni alama halali na sio vinginevyo.

Angalizo kwa wananchi ambao wameweka mazoea ya kuwa alama ya mkasi ni kwamba unamkataa mtu husika sio sahihi maana itachukuliwa kuwa ndiye unayemtaka na umemchagua. Anachotakiwa kujua mwananchi ni kwamba usiyemtaka unaacha wazi na kuweka alama kwa yule unayemtaka.

 Naye Afisa wa Tume ya Uchaguzi Flora Mkama akiwasilisha mada ya taratibu wa upigaji kura ufungaji wa vituturi na masanduku ya kura ikiwa ni pampja na  kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum mara wanapofika  katika eneo la kupiga kura, amesema kuwa ni lazima uwahakikishie   mawakala wa vyama vya siasa kwamba masanduku yapo wazi waridhike na mara uchaguzi unapokamilika kutumia vifungizi ambavyo vina namba maalum ambapo hakuna mtu anaweza kufungua mpaka masanduku yanapohitajika kufunguliwa kwa ajili ya kuhesabu kura mbele ya mawakala wa vyama hivyo  na wasimamizi wao husika.

Mkama amesema “Masanduku haya yana rangi tatu ambapo sanduku lenye mfuniko wa bluu wapiga kura wataweka kura za Rais, mfuniko mweusi kura ya Mbunge na mfuniko mweupe ni kura Diwani”

“Mpigakura anaweza kubadilisha uamuzi wake kwa kukabidhi karatasi ya awali kwa msimamizi ambaye ataweka karatasi husika kwenye bahasha maalum na kuhesabika kama kura iliyoharibika na atapewa karatasi nyingine ili kupiga kura yake”, amesema Nkama

 Nkama ameongeza kwa kusisitiza kuwa “Si hivyo tu bali sanduku la kura lina kambaambazo zina namba maalum (cereal number) za kufungia  upande wa kushoto, kulia na juu ya sanduku ambapo kila sanduku lina kamba hizo tatu ambazo haziingiliani na kamba za sanduku lingine na kuthibiti usalama wa masanduku husika”.

Naye Mkuu wa Kitengo cha leseni  za Mawasiliano katika  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania -TCRA  Mhandisi  Andrew Kisaka akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari  amesema kuwa makosa ya kimtandao yapo ya aina nyingi hususan katika mitandao ya kijamii kama vile online programmes, livestream, video clips (graphics designing) ambapo watendaji makosa wa mitandao wengi hawajajsajili na huweka taarifa ambazo sio sahihi mfano mtu anaweza kuchukua maneno ya mtu aliyoongea na kukata baadhi ya maneno na kutengeneza sentensi ambayo haikuwepo na kupotosha umma na kuharibu taswira ya mhusika hili ni kosa la jinai la kimatandao. Aidha, waandishi wa taarifa kwenye twitter, bloggers, facebook, instangram, na mengineyo ambao hawana taaluma ya uandishi ambapo huandika taarifa ambazo hazikusadifiwa pande zote zinazohusika na matokeo yake ni kuharibu taswira za wahusika (deformation)ambapo ni makosa ya jinai.

Akizungumzia suala la midahalo  amesema waandaaji wa vipindi maalum kama vile vya mahojiano, midahalo na masuala kama hayo, wanapashwa kutambua mdahalo wowote kwa wagombea wa ngazi yeyote ile ni lazima uwe na uwiano  kwa wagombea wote. Hii ikiwa na maana ni lazima kuuliza maswali sawa kwa wagombea wote, kila mmoja apewe muda sawa  wa kujieleza na chombo husika kihakikishe kinazingatia sharia, kanuni na taratibu za uchaguzi zilizowekwa bila kumuonea mgombea yeyote .

Aidha, vyombo vya habari vya binafsi vinaruhusiwa kutoza fedha sawa kwa wagombea na kuandaa vipindi vya mahojiano kwa wagombea mbalimbali bila kujali ukubwa wa chama utajiri au umasikini wa chama husika ili kuleta usawa na uwiano katika kutoa habari za wahusika. Kwa upande wa vyombo vya habari vya umma ni lazima kuzingatia sheria hizo, ila si ruhusa kutoza fedha kwa kuwa sio chombo cha biashara ukilinganisha na vyombo vingine.  

Akitoa wito kwa niaba ya Tume ya Uchaguzi Mkurugenzi Mwanga amewaomba wananchi wote wa Tanzania ifikapo tarehe 28, Oktoba 2020, siku ya Jumatano wajitokeze kwa wingi kwenda kwenye vituo vya kupigia kura ili kutimiza suala la kimsingi na kisheria la kupiga kura.  Mungu ibariki Tanzania

Post a Comment

Previous Post Next Post