Serikali Kutekeleza Ujenzi Wa Viwanja Vya Ndege Kigoma, Sumbawanga, Tabora Na Shinyanga

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amezindua miradi ya ukarabati na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Kigoma, Sumbawanga, Tabora na Shinyanga ambavyo vitagharimu kiasi cha Tsh. Billion 136 za kitanzania  zilizopatikana ndani ya kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European investment bank)  kwa mkopo wa masharti nafuu.

Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi kutoka Wizara ya Fedha, Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS),  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) , Wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa ambayo itaenda kunufaika na miradi pamoja na wakandarasi ambao wataenda kujenga viwanja hivyo.

Akizungumza katika uzinduzi huo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James  amesema, mradi huo ni mradi wa kimkakati unaolenga kutoa fursa kwa wananchi katika maeneo ya ujenzi na itaenda kuwa chachu ya maendeleo pia vitaenda kuongeza kasi ya ufanyaji wa biashara, kurahisisha mawasiliano, kuongeza viwango vya usalama  na kupelekea maendeleo kwa watu kwani vitatumika masaa 24.

“Mradi wa uboreshaji wa viwanja vinne vya ndege ni mradi wa kimkakati unaolenga kuvipa uwezo viwanja vya hivyo vya Mikoa ya Shinyanga, Rukwa (Sumbawanga), Tabora na Kigoma ili kuweza kutumia fursa nyingi zilizopo kwenye maeneo hayo na kukuza uchumi” Amesema Doto James

Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utakuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya uchukuzi, utalii, kilimo, pamoja na sekta ya Anga katika mikoa husika na nchi kwa ujumla ambapo wananchi wataenda kufaidika na fursa mbalimbali ambazo zitazalishwa kupitia viwanja hivyo.

Aidha, Doto amewasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanamaliza ujenzi katika muda uliopangwa kwa sababu Wizara yake haitovumulia ucheleweshwaji wowote utakaojitokeza  na wamejipanga vizuri kufuatilia kwa karibu mwenendo wote wa ujenzi ili kuhakikisha unamalizika kwa wakati kwa sababu viwanja hivyo vinahitajika sana hasa wakati huu ambapo Tanzania imejiimarisha katika usafiri wa Anga pamoja na Sekta ya Utalii.

“Naomba kusisitiza, sasa hivi tupo kivingine sana hasa sisi Wizara ya Fedha na Mipango, ile habari ya kuongeza muda wa utekerezaji wa miradi unatakiwa kuwa umejiandaa sawasawa kwa sababu tutauliza mpaka  tulidhike na tutafuatilia kwa ukaribu sana, Wale waliopewa miezi 12 wahakikishe mradi unakamilika ndani ya muda huo, na wale wa miezi 18 wahakikishe wanamaliza kwa wakati, viwanja hivi vya ndege tunavihitaji sana” amesema Mhe. Dotto james

Akizungumza katika hafla hiyo Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi  Patrick Mfugale  ameeleza kuwa, ukarabati  na ujenzi utakaofanyika katika viwanja hivyo ni pamoja na ujenzi wa majengo ya abiria, ujenzi wa majengo ya kuongozea ndege, maegesho ya magari , uzio wa usalama, maegesho mapya ya ndege, barabara ya magari ya kuingia uwanja wa ndege, barabara ya kuruka ndege pamoja na usimikaji wa mitambo ya umeme ambapo baada ya ujenzi na ukarabati kukamilika viwanja hivyo vitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa kama,  Bombadia na  Airbus

Ameongeza kuwa TANROADS  na Wizara ya Ujenzi itasimamia na kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa viwanja hivyo na kuhakikisha vinamalizika kwa wakati na vinaanza kuwahudumia wananchi wa maeneo husika ili wakanufaike na viwanja kwa kukuza uchumi wao ambao utaimarika kupitia masoko ya kuuza mazoa kwa  watu kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi. 

“Sisi kama TANRODAS na Wizara ya Ujenzi tutahakikisha tunasimamia na tunaahidi kuwa tutafuatilia kwa ukaribu miradi hii ili ikalete tija kwa wanufaika katika maeneo ya Kigoma, Rukwa(Sumbawanga), Tabora na Shinyanga” Amesema, Mhadisi Mfugale

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ambayo ujenzi wa viwanja hivyo unaenda kufanyika Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Rashidi Mchaka ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa viwanja hivyo kwani mwanzoni havikuwa na hali nzuri  lakini kwa marekebisho yatakayofanyika vitaenda kuimarisha sekta ya mawasiliano na kupelekea maendeleo ya uchumi katika Mikoa hiyo.

“Shughuli hii ni muhimu sana katika mikoa yetu ya pembezoni ambayo ni Shinyanga, Tabora, Rukwa (Sumbawanga) na Kigoma, hali ya viwanja haikuwa nzuri sana na kama ilivyoelezwa mipango iliyoko hapa itaimarisha katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi na mawasiliano katika mikoa yetu.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa tatu kulia), akikata utepe ikiwa ni alama ya kuzindua rasmi ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, utakaogharimu Euro milioni 50 sawa na Sh. bilioni 136.85 zikiwa ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), katika ukumbi wa Benki Kuu Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, Mkurugenzi wa Miundombinu TAMISEMI Mhandisi Gilbert Mwoga na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege -TAA, Bw. Hamisi Amiri.

Post a Comment

Previous Post Next Post