NEC,IMETEKELEZA WAJIBU WAKE MCHAKATO MZIMA UCHAGUZI MKUU 2020

 

Na.Paschal Dotto-MAELEZO.

Katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa Mamlaka iliyopewa kikatiba ya kuratibu na kusimamia shughuli  zote za uchaguzi, ilianza mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa mwaka 2020 kwa kuhuisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Katika Mchakato huo ambao ulifanyika katikati ya mwaka 2019 na uzinduzi rasmi ulifanyika katika Mji wa Moshi Mkoani Kilimanjaro Julai 18, 2019, ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa  alikuwa mgeni rasmi na kuzindua daftari hilo ambalo lina wapiga kura halali 29,188,347, wanaotegemea kupiga kura katika vituo 80,155 kwa Tanzania Bara.

Mchakato huo ulioanza mapema 2019, uliwashikisha  wananchi wanaostahili kupiga kura ambapo waliitikia vyema kwa kujiandikisha ili kutimiza haki yao kikatiba ya kuwachagua viongozi ambao  watawaongoza katika miaka mitano.

NEC, Iliingia mchakato mwingine ambao ulikuwa ni kupiga kipenga na  kuviandaa vyama vya siasa katika kushiriki huo,  ambapo  Julai 21, 2020, Mwenyekiti wa NEC Jaji (Mst) Semistocles Kaijage alitangaza rasmi mchakato wa uteuzi wa wagombea wa Urais, Ubunge, Udiwani ambao ulikuwa Agosti 25 na ule wa kampeni wa Agosti 26 mpaka 27 Oktoba, 2020, hatimaye tukio lenyewe ambalo alisema litafanyika Oktoba 28, 2020. 

Aidha, NEC ilisisitiza kuwepo kwa kampeni za kistarabu kwa vyama vya siasa kwa kuzingati amani na utulivu kwa wananchi wote, wanasiasa kuhubiri mshikamano na umoja, ambapo kwa kiasi kikubwa mpaka sasa vyama vya siasa vinaelekea tamati kwenye kampeni zao baada ya kunadi sera na kuacha kazi kwa wananchi ambao wataamua sera za chama kipi zilikuwa na mvuto na kuweza kuchagua viongozi wa chama hicho

Tume ilingia kwenye mchakato mwingine wa kukutana na  watu wenye mahitaji  maalum kama vile walemavu ambapo kwa mara ya kwanza NEC imewaangalia kwa karibu kundi hilo ili waweze kupata haki yao kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Katika Kutekeleza hilo, NEC iliaendaa jarada la nukta nundu ambalo limeboreshwa kwa kiasi kikubwa litawasaidia wapiga kura wenye uhitaji maalum hasa wasioona, kwa hiyo  nao watapata haki yao bila kurubuniwa na watu ambao wataambatana nao kwenda kwenye vituo vya kupigia kura.

NEC, ilitekeleza mchakato mwingine wa kukutana na Wahariri pamoja na Waandishi wanaoandaa maudhui  mtandaoni na kuwaelimisha jinsi ya kuripoti matukio ya uchaguzi kuanzaia kampeni mapaka kupiga kura na matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2020.

Hapa, NEC iliazimia kutoa mafunzo kuhusu uchaguzi, ambapo kwa mara ya kwanza iliwahusisha waandishi wa habari za mitandao lakini pia na  vyombo vya habari vyote vikuu na ilitoa utaratibu ni namna gani wanatakiwa kuripoti bila kulete mkanganyiko au maneno yenye kuashiria uchochezi unaoweza kuvuruga uchaguzi na kuleta adha kwa wananchi.

Oktoba 15, 2020, NEC ilihakikisha Uchaguzi wa 2020 unakuwa wa huru na haki kwa kukabidhi Nakala Tepe ya Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa vyama 19 vinavyoshiriki uchaguzi wa mwaka huu lenye wapiga kura halali 29,188,347.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dkt.Wilson Mahera alisema kuwa daftari hilo lina majina, picha  na takwimu za wapiga kura ambao wako halali katika kutekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kuchagua viongozi wao watakaowaongoza kwenye miaka mitano ijayo.

Katika tukio hilo, NEC pia ilikabidhi nakala ya vituo vya kupigia kura kwa Tanzania bara ambapo alisema kuwa kuna vituo 80,155 nchi nzima na  vitatumika kihalali Oktoba, 28, 2020 kwa kuwawezesha wananchi kutekeleza wajibu wao wa kuwachagua viongozi.

Pia, NEC walikabidhi  mfano wa karatasi ya kupigia kura kwa nafasi ya urais pamoja na jarada la nukta nundu ambalo litatumika kwa watu wenye mahitaji maalum hususani kwa wenye tatizo la kutoona ambao nao wamepewa haki yao  ya  kutekeleza vizuri zoezi hilo ambalo linawapa wananchi nafasi ya kupata viongozi wanaowataka.

NEC, ilitekeleza mchakato mwengine safari hii ulihusu moja kwa moja vyombo vikuu vya Habari, ambapo ilitoa semina ya siku mbili kuanzia Oktoba 20-21, 2020 na  iliwaeleza wanahabari namna uwazi unavyokuwa kwenye Chaguzi za Rais, Wabunge na Madiwani.

NEC, ilihakikisha Wanahabari  wanakuwa mabalozi wazuri wa kuwaeleza wananchi jinsi uwazi na haki inavyotendeka kwenye mchakato mzima wa uchaguzi, hapa NEC ilifanya uchaguzi wa mfano, ambapo Wanahabari walipiga kura kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani katika majimbo ya mfano, Twiga na Nyati na vyama vya Orange Union, Nanasi Allince na Apple Democratic vishiriki  Uchaguzi huo huku Chama cha Orange Union kikiibuka na ushindi wa kiti cha Urais.

Lengo la Uchaguzi huo, lilikuwa ni kuwaelimisha wanahabri ili wapeleke ukweli  kuhusu mchakato wa uchaguzi ambao wananchi hawaufahamu, lakini pia NEC walieleza namna fomu namba 18 na 19 inayotumika kwa watendaji wa uchaguzi hususani Wasimamizi na mawakala wa uchaguzi wakijaza fomu hiyo inawapa haki ya kupiga kura tofauti na kituo chao walichojiandisha, huku fomu namba 19 ikiwahusu viongozi wanaotoka sehemu tofauti na walikojiandisha hupewa fomu hiyo.

Aidha, NEC ilikutana na Viongozi wa Dini katika Mkutano uliofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere  (JNICC), Jijini Dar es Salaam, ambapo Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dkt.Wilsoni Mahera aliwahakikishia kuwepo kwa uchaguzi wa uhuru na haki na wananchi watapata nafasi nzuri ya kuchagua kiongozi kutokana na sera zilizonadiwa kwa kipindi cha miezi cha kampeni ambazo zitahitimishwa Oktoba 27, 2020, na maamuzi yatafanyika katika Uhuru, Uwazi, Upendo na Haki.

Mwisho.  

Post a Comment

Previous Post Next Post