VIONGOZI WA DINI MKOANI SINGIDA WAJA NA MAAZIMIO SABA UCHAGUZI MKUU

 


  Mwenyekiti wa Kamati ya  Amani ya Viongozi wa Dini  na Madhehebu mbalimbali Mkoa wa Singida,(aliyesimama)Hamis Muhamed Kisuke akiongoza kikao ambapo walizungumzia  hali ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu na kuja na maazimo saba. (Picha na Rose Nyangasa).

Mkuu wa Mkoa  wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi  akizungumza na Kamati  ya Amani ya Viongozi wa Dini na Madhehebu  mbalimbali Mkoa wa Singida ambapo ameipongeza Kamati hiyo kwa kuamua  kuhamasisha amani na utulivu kwenye  kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu (Picha na Rose Nyangasa)

 Wajumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Singida wakimsikiliza kwa makini Kamanda wa Polisi wa MKoa wa Singida, Sweetbert Njewike (hayupo pichani) wakati akielezea majukumu ya jeshi hilo kwenye siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Rose Nyangasa).

      Kamanda wa Polisi wa MKoa wa Singida, Sweetbert Njewike majukumu ya jeshi hilo kwenye siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Rose Nyangasa).

 

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Kamati ya Amani na Dini mbalimbali  Mkoa wa Singida inayojumuisha viongozi wa madhehebu na dini zote  imetoa tamko lenye maazimio saba kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba  28, mwaka  huu huku  ikiwaomba waumini wao kumtanguliza Mungu na Serikali kusimamia  amani na utulivu ili kuwapata viongozi bora watakaoingoza  nchi katika miaka mitano ijayo 2020 hadi 2025.

Akisoma maazimio hayo, Mwenyekiti wa  Kamati hiyo Shehe, Hamis Muhamed Kisuke amesema  miongoni mwa maazimio hayo ni  kuwaomba waumini wao kutenga siku tatu kuanzia Ijumaa hadi Jumapili ya juma hili kwa ajili ya  kufunga na kuomba ili kuombea  uchaguzi upite  kwa  amani na usalama.

Maazimio mengine  yaliyofikiwa kwenye kikao hicho ni pamoja na viongozi wa dini katika kipindi hiki kudumisha  Amani, kutotumika  kwenye majukwaani ya siasa kushabikia  viongozi wa vyama vya siasa, kuhubiri Amani,

kuhimiza waumini wao kushiriki kupiga kura na kuhimiza kufuata na kutii sheria za  nchi ambapo  pia wamesisitiza kuviacha vyombo  halali vilivyopewa dhamana  ya kusimamia uchaguzi huo vifanye kazi yake.

Mwakilishi wa dini ya Kiislam (Baraza la Kiislam Tanzania) katika  Mkoa wa Singida Shehe, Issa Nassor amesema Amani  ikitoweka  watakaoumia  zaidi ni  watoto, wanawake, wajawazito, wazee na watu wenye  mahitaji maalum kwa kuwa  hawana  uwezo wa  kukimbia  na kujitetea.

Aidha,  wamewataka wazazi  na walezi wa kila familia  kuwaasa  vijana kujiepusha  na kushawishiwa na watu wanaoitakia  mabaya  nchi ya Tanzania ambapo ameongeza kwamba   baada ya  kupiga kura vijana warejee  nyumbani  kwa  kuwa tayari Serikali imeshaweka  vyombo maalum kwa ajili  kuhesabu na kutangaza matokeo hayo.

“Historia inaonyesha kuwa nchi zote duniani zilizopoteza amani ni nchi ambazo walilewa amani, vilevile tukumbuke kupata amani ni mchakao wakati  kuvunja amani  ni jambo rahisi  kabisa. Nawaomba watanzania wenzangu  kutumia  vipande  vyetu vya kupigia kura  kuwachagua Viongozi bora” aliongeza  Shehe, Nassor

Mwakilishi kwa upande wa wakristo, Askofu wa Kanisa la TAG mkoani Singida, Gasper Mdimi amesema amani  ya nchi ni jambo nyeti ambalo linatakiwa  kuchukuliwa  kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa  lina athari   pana  kuanzia  kwenye  ngazi ya  kaya  hadi taifa kwa ujumla  na kwamba  Bibilia imefafanua  kuwa chanzo cha Amani  ni  Mungu mwenyewe, Haki na Watu wanaomcha  Mungu.

Amefafanua kuwa  vitabu vyote vitakatifu  vinasisitiza kutafuta  kuwa na amani  na watu wote ambapo   na kwamba watanzania  wanatakiwa kupendana  katika kipindi hiki bila kuangalia   vyama vyao  vya  Siasa   na kuiombea  nchi yao  ipate  viongozi ambao  watailinda amani.

Pia amesema   wakati  wananchi wanakwenda  katika siku za mwisho wa kuhitimisha zoezi la kuwachagua viongozi   ni  muhimu  kuzingatia kuacha kuongea  maneno ambayo yatasababisha machafuko na  uvunjifu wa amani.

Mwakilishi wa Mhashamu Baba Askofu wa  Jimbo  Katoliki la Singida, Padre Padri Elia Mnyakanka amesema Uongozi Bora ni tunu na zao  la amani na kwamba  ili kuwa na maendeleo na ustawi  kuanzia ngazi ya familia na taifa ni muhimu kwa wananchi kutafakari kwa kina  na kuwachagua viongozi wanaoweza kuilinda amani.

Akitoa mfano amesema katika taifa la Israel uongozi bora ulikuwa ni nyenzo ya kuwafikisha  kwenye nchi ya ahadi kupitia manabii mbalimbali ambapo kwa kufanya hivyo amani ilipatikana.

Amesema  viongozi wa dini wanapaswa  kuwapa elimu ya uraia waumini wao  ili kuwapa  uwezo  wa kuwachagua wagombea makini kupitia ilani zao ambapo amesisitiza kwamba uchaguzi wa haki na amani ndiyo njia pekee ya kujitawala na kuleta amani katika nchi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida,  Sweetbert Njewike  amesema kwenye kipindi hiki  cha uchaguzi majukumu yao  ni pamoja na  kutunza na kudumisha Amani, kusimamia utekelezaji wa sheria, kuzuia na kubaini makosa ya jinai, kuwakamata wahalifu wanaohatarisha amani na kuwafikisha katika vyombo vya sheria, kulinda  mali za raia, kutoa ulinzi kwa maafisa na vituo, pia kuhakikisha hakuna mtu anaye watishia wapiga kura na kuhakikisha usalama wa vifaa vya kupigia kura. 

Mkuu wa Mkoa Singida Dkt.Rehema Nchimbi amewashukuru viongozi hao kwa kuandaa mkutano  huu ambao umelenga kudumisha amani na kuwahimiza wananchi washiriki kikamilifu kupiga kura  ili kuwa chagua viongozi bora.

Aidha Dkt.Nchimbi amewataka Viongozi wa Dini kutotumika kuharibu amani na mshikamano ambao  upo kwa kipindi kirefu sasa hapa nchini kutokana na kazi nzuri  ya kusimamia amani hiyo iliyofanywa na Serikali

Post a Comment

Previous Post Next Post