Mwandishi Wetu,Dodoma
Ushirikiano baina ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani Kilimo (NAESA) unatarajiwa kuimarisha huduma za ugani, kuongeza matumizi sahihi ya mbolea na hatimaye kuinua tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini.
Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha pamoja kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, na Kaimu Mtendaji Mkuu wa NAESA, Dkt. Wilhelm Leonard Mafuru, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za NAESA, NANENANE–Nzuguni, jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema taasisi hizo zina majukumu yanayokamilishana katika kuendeleza sekta ya kilimo na kwamba ushirikiano huo utaimarisha utoaji wa huduma kwa wakulima nchini.
Laurent amesema ushirikiano huo utajumuisha utoaji wa mafunzo kwa maafisa ugani, uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea, uanzishwaji wa mashamba darasa na utoaji wa elimu kuhusu afya ya udongo ili kuongeza tija ya uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa NAESA, Dkt. Wilhelm Leonard Mafuru, amesema ushirikiano huo utafungua ukurasa mpya wa kuimarisha utendaji wa taasisi hizo kwa lengo la kumfikia mkulima moja kwa moja kupitia huduma bora za ugani.
Dkt. Mafuru amesema matumizi ya mifumo ya pamoja yatawawezesha maafisa ugani kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuongeza ushirikiano katika utoaji wa elimu, maarifa na ubunifu utakaochangia kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Viongozi hao walisisitiza kuwa ushirikiano kati ya TFRA na NAESA utakuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha wakulima wanapata huduma bora za ugani, mbolea zenye ubora unaotakiwa pamoja na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, hatua itakayochangia maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo nchini.







