SERIKALI YAWAPA WANAFUNZI 1,050 UFADHILI WA SAMIA SCHOLARSHIP


 Serikali imetangaza orodha ya wanafunzi 1,050 waliofanya vizuri zaidi katika Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2026 watakaonufaika na mpango wa Samia Scholarship, ambapo wanafunzi 50 bora zaidi watapelekwa kusoma nje ya nchi katika fani za Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), Data Science na teknolojia nyingine za kisasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Julai 27, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema mpango huo unatekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ukiwa na lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) ili kuzalisha wataalamu watakaochochea maendeleo ya taifa.

Profesa Mkenda amesema kati ya wanafunzi hao, 1,000 watapata ufadhili wa kusoma katika vyuo vikuu vya ndani, huku wanafunzi 50 bora zaidi wakipewa nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi katika fani zinazohitajika katika uchumi wa kidijitali.

Amefafanua kuwa wanafunzi hao wamepatikana kutoka katika tahasusi za PCM (Physics, Chemistry and Mathematics), PCB (Physics, Chemistry and Biology), CBG (Chemistry, Biology and Geography), PMG (Physics, Mathematics and Geography), CBA (Chemistry, Biology and Agriculture) pamoja na PMC (Physics, Mathematics and Computer Science).

Kwa mujibu wa Waziri huyo, wanafunzi watakaonufaika na ufadhili wa ndani wanatakiwa kuomba udahili katika vyuo vikuu vya Tanzania kusomea shahada za Hisabati, Sayansi, Uhandisi au Tiba. 

Baada ya kupata nafasi ya masomo, watajaza fomu ya kujiunga rasmi na mpango wa Samia Scholarship, huku Serikali ikigharamia masomo yao kwa asilimia 100.

Aidha, amesema majina ya wanafunzi wote waliochaguliwa yamechapishwa kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuwataka wahitimu wa Kidato cha Sita kuyakagua na kufuata taratibu zilizowekwa ili kukamilisha mchakato wa kupata ufadhili huo.

Akizungumzia wanafunzi 50 bora zaidi watakaopelekwa nje ya nchi, Profesa Mkenda amesema wameteuliwa kutoka katika tahasusi za PCM, PMG na PMC, ambazo zinahitaji umahiri mkubwa wa Hisabati ya Juu (Advanced Mathematics).

Amesema uteuzi umezingatia alama halisi za mtihani badala ya daraja la ufaulu pekee, akieleza kuwa wanafunzi wengi wanaweza kupata daraja la “A” lakini wakatofautiana kwa idadi ya alama walizovuna.

Profesa Mkenda amesisitiza kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa katika uwazi na uadilifu wa mchakato huo ili kulinda hadhi ya Samia Scholarship. 

 

Amesema mwanafunzi yeyote mwenye mashaka kuhusu kutokuwamo kwenye orodha anaweza kuwasiliana na Wizara kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa alama zake kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).

Pia amebainisha kuwa asilimia 58 ya wanafunzi waliochaguliwa wametoka katika shule za serikali, huku asilimia 42 wakitoka katika shule zisizo za serikali, akisisitiza kuwa uteuzi umefanyika kwa kuzingatia vigezo vya ufaulu bila kujali aina ya shule aliyosoma mwanafunzi.

Waziri Mkenda amewataka wanafunzi wote waliopata nafasi hiyo kuitumia kwa bidii, nidhamu na uzalendo, akieleza kuwa uwekezaji huo wa Serikali unalenga kujenga kizazi cha wataalamu kitakachoiwezesha Tanzania kushindana kimataifa katika sayansi, teknolojia na ubunifu.  

Post a Comment

Previous Post Next Post