TFRA ,TOAM KUKUZA MATUMIZI YA MBOLEA HAI NCHINI

Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Taasisi ya Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kukuza matumizi ya mbolea hai nchini kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao na kuendeleza kilimo endelevu kinacholinda mazingira.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, ambapo pande hizo mbili zilijadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano yatakayochochea maendeleo ya tasnia ya mbolea hai na kuongeza uelewa kwa wadau wa kilimo nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Laurent alisema TFRA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha matumizi ya mbolea hai yanaongezeka kupitia utoaji wa elimu, uhamasishaji kwa wakulima na kujenga uwezo wa wazalishaji wa mbolea hizo ili kukidhi mahitaji ya soko.

Aidha, pande hizo mbili zilijadili namna ya kusaidia viwanda vinavyozalisha mbolea hai katika masuala ya usajili na upimaji wa ubora wa bidhaa zao, pamoja na kuboresha ukusanyaji na upatikanaji wa takwimu za uzalishaji na matumizi ya mbolea hai nchini.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza matumizi ya mbolea hai, kuimarisha uwezo wa wazalishaji, kuongeza tija ya kilimo na kuchangia maendeleo ya kilimo endelevu kwa manufaa ya wakulima na taifa kwa ujumla.


Post a Comment

Previous Post Next Post