WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imepanga kujenga madarasa 1,360 kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa sera ya elimu ya miaka 10 ya lazima sambamba na kuongeza miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari nchini.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha mazingira ya elimu na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za elimu kwa wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali itajenga mabweni 17 katika shule za sekondari 17 pamoja na nyumba 33 za walimu ili kuboresha mazingira ya kazi na makazi kwa walimu, hususan katika maeneo yenye changamoto za miundombinu.
Vilevile, vituo 50 vya walimu vitajengwa katika Halmashauri za Wilaya kwa lengo la kuongeza motisha kwa walimu na kusaidia utoaji bora wa huduma za elimu.
.jpeg)