Wadau michezo na wanamichezo nchini wamehimizwa kutumia huduma za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kusajili kazi zao za ubunifu na kujifunza kuhusu haki zao ili kuleta tija na ufanisi wa wanamichezo kwa kuwakomboa kiuchumi.
Wito huo umetolewa tarehe 08 Mei, 2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Salvio Kapinga wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu Duniani iliyofanyika hoteli ya Hyatt Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Judith Kapinga alisema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhahikisha wanamichezo na wadau wa sekta hiyo wanatumia Miliki Ubunifu kukuza tasnia ya michezo hapa nchini.
“Niwasihi viongozi wa vilabu vya michezo, mashirikisho na wadau wote wa michezo kuwasaidia wanamichezo katika vilabu na mashirikisho yenu kuhakikisha wanalinda haki zao ikiwemo matumizi ya picha au taswira zao katika bidhaa au biashara za watu wengine,’’ alisema Bi. Judith Kapinga.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA Prof. Neema Mori alisema ni muhimu wadau wa michezo wakajiepusha kabisa kutumia Miliki Ubunifu kama vile Alama za biashara (logo) zisizo zao pasipo idhini ya wamiliki halisi ili kuepuka kuingia katika matatizo ya kisheria kwa kutumia Alama zilizosajiliwa na watu wengine.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa aliwakumbusha wadau na wanamichezo kutumia majina yao vizuri ‘Brand Names’ kujiandaa na maisha mengine baada ya kustaafu michezo.
“Naomba nitoe mifano michache kwa wachezaji wa kimatiafa wanaoendelea kunufaika kwa kutumia Alama za Biashara ingawa wengine wameshajiuzulu michezo, Alama ya biashara (logo) ya CR7 inayomilikiwa na mchezaji wa mpira wa miguu Christiano Ronaldo ni Dola za Kimarekani Milioni 900,” alisema Nyaisa.
Kwa upande mwingine Mwenyeki wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mhandisi Leodigar Tenga alisema wakati taifa likiwa kwenye maandalizi ya AFCON 2027 ni vyema wafanyabiashara na wadau wote wa michezo wakahakikisha wamelinda bunifu zao ili kuepuka wizi na uharamia kwenye bidhaa na huduma kwa upande wa matumizi ya Alama (brands) zilizopata umaarufu na ambazo ni bora.
Maadhimisho ya Miliki Ubunifu na Utoaji wa Tuzo za Miliki Ubunifu kwa wadau wa michezo mwaka huu yamefanyika yakiwa na kauli mbiu isemayo “Miliki Ubunifu na Michezo; Jitayarishe, Jipange, Vumbua.”




