MASVINGO – ZIMBABWE
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Sita (6) wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Usimamizi wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi unaofanyika Masvingo, Zimbabwe.
Aidha, Mkutano huo pamoja na masuala mengine umejadili maendeleo yaliyopatikana katika utekelezaji wa programu za kikanda na masuala ya kimkakati katika utekelezaji wa afua mbalimbali katika Usimamizi wa maafa,pia mkutano huo utatumika kama jukwaa kwa Mawaziri kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo wa Kimataifa na Jumuiya ya Wafadhili kuhusu uwekezaji katika Usimamizi wa Maafa ili kujenga ustahimilivu wa kikanda.
Naibu Waziri Ameongozana na mwenyeji wake ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Mhe. CP-Suzan Kaganda, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jenerali Hosea Ndagala, Mkurugenzi Msaidizi Urasimishaji Makazi kutoka ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Nicholaus Mwakasege, Mratibu wa Maafa Dkt. Baltazar Leba, Bw. Abubakar Juma kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Msaidizi wa naibu waziri Bw. Blastus Kahemela, Msaidizi wa katibu mkuu Bw. Januari Kitunsi, pamoja na afisa habari Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Nyamagory Kitwara.





