
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi amekutana na kufanya mazungunmzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la CAN Tanzania, Dkt. Dk.Sixbert Mwanga.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Mei 14, 2026 katika Ofisi ndogo ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Luthuli Jijini Dar es Salaam viongozi hao walijadiliana kuhusu mchango wa nishati jadidifu katika ukuaji wa uchumi.
Katika maelezo yake, Dkt. Muyungi amesema Ofisi yake imefungua milango ya ushirikiano na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi ili kuhakikisha masuala ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi inapiga hatua.
“Kwa kipindi hiki tumefungua zaidi milango ya ushirikiano na wadau wa sekta binafsi ili tuweze kupiga kubwa zaidi kuhusu masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia jamii na taifa kwa ujumla amesema Dkt. Muyungi.
Aidha Dkt. Muyungi amebainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ipo katika maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo ni wajibu wa wadau kushirikiana na Serikali katika kuweka mazingira wezeshi na hivyo kufikia malengo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CAN Tanzania, Dkt. Sixbert Mwanga ameishukuru Ofisi ya Makamu kwa kuendelea kushirikiana na shirika hilo katika utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.