Jukwaa la Tanzania na Urusi laibua fursa mpya za uwekezaji katika kilimo

Mwandishi Wetu,

Fursa za uwekezaji katika tasnia ya mbolea na maeneo mengine ya kimkakati zimejadiliwa katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi (Tanzania–Russia Trade and Investment Forum) lililofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha, likiwakutanisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema mbolea ni nyenzo muhimu katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini, hivyo kuna fursa kubwa za uwekezaji katika tasnia ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.

Mhe. Kombo amesema hayo wakati wa majadiliano yaliyowakutanisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Urusi, yakilenga kuibua fursa mpya za ushirikiano katika sekta mbalimbali za uchumi.

Aidha, jukwaa hilo limeweka mkazo katika maeneo ya kilimo, madini, viwanda, nishati, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na elimu ya ufundi, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuongeza uzalishaji wenye tija.

Katika jukwaa hilo, watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walishiriki na kufuatilia kwa karibu mijadala kuhusu fursa za ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta ya kilimo na pembejeo za kilimo, hatua inayotarajiwa kuchochea uwekezaji na maendeleo ya tasnia ya mbolea nchini.


Post a Comment

Previous Post Next Post