Serikali Yaelekeza Kuongeza Uzalishaji wa Mbolea Asili

Mwandishi Wetu,

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Peter Msofe, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufanya mazungumzo na wakurugenzi wa halmashauri na majiji ili kuweka utaratibu wa kukusanya na kusambaza taka zinazozalishwa mijini kwa wazalishaji wa mbolea za asili, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kutosha kwa viwanda hivyo. 

Aidha, Naibu Katibu Mkuu ameisisitiza TFRA kuwa na takwimu sahihi za uzalishaji na matumizi ya mbolea za asili ili kusaidia katika maandalizi ya taarifa za kiserikali na upangaji wa sekta ya kilimo.

Katika hatua nyingine, Prof. Msofe ameipongeza TFRA kwa juhudi zake za kuhamasisha matumizi ya mbolea, akibainisha kuwa wakulima wengi wameanza kuona tija ya matumizi sahihi ya pembejeo. Hata hivyo, ameisisitiza mamlaka kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya wakulima.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent,  amesema matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 363,145 mwaka 2020/2021 hadi tani 972,074 mwaka 2024/2025, huku yakitarajiwa kufikia tani 1,031,313 kufikia Juni 2026.


Post a Comment

Previous Post Next Post