Mwandishi Wetu,
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Rose Mihayo, amesema kuwa hati za kimila zina umuhimu mkubwa kwa wakulima kwani zinawawezesha kumiliki rasmi mashamba yao na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Mihayo alitoa kauli hiyo leo, tarehe 25 Machi 2026, wakati wa zoezi la ugawaji wa hati za kimila lililofanyika katika Kata ya Usagali, wilayani Nzega, ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Nzega DC) walikabidhi hati hizo kwa wakulima.
Ameeleza kuwa, kupitia hati hizo, wakulima watapata taarifa sahihi za ukubwa wa mashamba yao, hali itakayowasaidia kupata ruzuku mbalimbali za Serikali ikiwemo mbolea na mbegu bora, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha kama benki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji, Bw. Joseph Mihambo, ameishukuru TFRA kwa kuratibu na kusimamia zoezi hilo, akibainisha kuwa hatua hiyo itachochea maendeleo ya kilimo katika kata hiyo na kuongeza tija kwa wakulima.
Zoezi hilo la ugawaji wa hati za kimila lina lengo la kuwawezesha wakulima kumiliki ardhi kisheria, kuboresha uzalishaji wa mazao wanayolima na kuchangia maendeleo ya uchumi wa wananchi wa Nzega vijijini.


