SERIKALI YAONGEZA MSISITIZO KUDHIBITI USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA (UVIDA)

 

Serikali imeongeza msisitizo wa kuimarisha juhudi za kudhibiti usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA), kwa kuhimiza wizara na taasisi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mpango mkakati wa pamoja chini ya mwavuli wa Afya Moja (One Health Approach).

Hayo yamesemwa leo, Machi 31, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha 32 cha Kamati ya Kitaifa ya uratibu wa masuala ya UVIDA inayojumuisha wizara mbalimbali chini ya mfumo wa Afya Moja. 

Akiongea wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema kuwa wajumbe walipokea na kujadili taarifa kutoka katika kamati tendaji tano zinazoshughulikia maeneo tofauti ya udhibiti wa UVIDA, zikiwemo kamati ya uelewa na uhamasishaji wa umma, kamati ya ufuatiliaji wa maabara na uchunguzi, kamati ya kinga na udhibiti wa maambukizi (IPC), kamati ya usimamizi wa matumizi sahihi ya dawa pamoja na kamati ya ufuatiliaji na tathmini.

Dkt. Magembe amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila wizara na taasisi husika kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kudhibiti UVIDA sambamba na kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa, kuboresha usimamizi na kuhakikisha mikakati ya kitaifa inatekelezwa kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Katibu wa kikao hicho ambaye pia ni Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi, amesema kuwa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa unaendelea kuwa tishio kubwa kwa nchi nyingi duniani, hivyo Tanzania inapaswa kuweka juhudi madhubuti za kujilinda dhidi ya athari zake.

Aidha, kikao hicho kimesisitiza umuhimu wa kuongeza uhamasishaji kwa jamii pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa dawa ili kupunguza matumizi yasiyo sahihi yanayochangia kuongezeka kwa usugu wa vimelea vya magonjwa.

Wajumbe wa kikao hicho pia wamekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu katika ngazi zote ili kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa wakati, hatua itakayosaidia kulinda afya ya jamii na kuimarisha mfumo wa afya nchini kwa ujumla.       

Post a Comment

Previous Post Next Post