PROF. SHEMDOE AAGIZA MAANDALIZI YA MAPEMA KUPOKEA MAKUNDI RIKA MAWILI YA WANAFUNZI WA KIDATO CHA KWANZA 2028

Mwandishi Wetu,

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof.Riziki Shemdoe, amewaelekeza Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri kuanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya kupokea makundi rika mawili (double cohort) ya wanafunzi wa Darasa la Sita na la Saba watakaohitimu masomo yao mwaka 2027 na kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2028 kwa pamoja.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo  Machi 2, 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 12 wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara unaofanyika katika Ukumbi wa Lush Garden Hotel, jijini Arusha.

“Tuanze maandalizi ya mapokezi ya Darasa la Sita na  la Saba ambao wataingia Kidato cha Kwanza kwa pamoja  Januari 2028,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Ameeleza kuwa Maafisa Elimu wanazo takwimu sahihi za wanafunzi hao, hivyo wanapaswa kuziandaa kwa umakini na kuziwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwezesha maandalizi maalumu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa, upatikanaji wa madawati na ajira ya walimu wa kutosha.

Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na madiwani, wazazi na walezi kuendelea kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya awali, msingi na sekondari wanapata chakula shuleni ili kuboresha mahudhurio na ufaulu wao.


Post a Comment

Previous Post Next Post