
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
20/3/2026 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao katika kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayofanyika katika tawi lake lililopo Soko Kuu la Kariakoo, ghorofa ya tano jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa karibu na wananchi hususan wafanyabiashara wa Kariakoo na wakazi wa maeneo ya jirani.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo alisema kambi hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwahamasisha kupima afya zao mara kwa mara hasa vijana ambao kwa sasa wako katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo kutokana na mtindo usiofaa wa maisha ikiwemo matumizi ya pombe, sigara na lishe duni”, alisema Dkt. Kisenge.
“Ninawaomba wananchi mbadili mtindo wa maisha kwa kuacha uvutaji wa sigara, kupunguza matumizi ya pombe kupita kiasi, kula lishe bora na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepuka magonjwa hatari kama kiharusi na kisukari”, alisema Dkt. Kisenge.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi kufahamu namba zao za afya ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari, uzito, urefu na kiwango cha mafuta mwilini ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yanayoongezeka kwa kasi.
“Tunaposema ‘Jua Namba Zako’ tunamaanisha kila mmoja ajue uzito wake, urefu, sukari, mafuta mwilini na mapigo ya moyo. Ufahamu huu ni kinga muhimu dhidi ya magonjwa yanayosababisha vifo vya ghafla”, alisisitiza Dkt. Kisenge.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima afya zao walieleza kuridhishwa na huduma hiyo na kuitaja kuwa msaada mkubwa kwa jamii.
Hamisi Rashidi mkazi wa Mbagala Zakheem, alisema alipogundua uzito wake hauendani na urefu wake alipatiwa ushauri wa kufanya mazoezi ili kuboresha afya yake.
“Naishukuru JKCI kwa huduma hii. Waendelee kutoa elimu ili wananchi wapate taarifa sahihi kutoka kwa wataalamu badala ya kuamini uvumi kutoka kwa watu ambao siyo wataalamu wa Afya”, alisema Rashidi.
“Kambi hii imenisaidia kuelewa zaidi dalili za magonjwa ya moyo na umuhimu wa kupima afya mara kwa mara. Huduma hii ni muhimu sana kwa sababu iko karibu na maeneo yetu ya kazi, imenirahisishia kupima na kupata ushauri wa kitaalamu kwa wakati”, alisema Amina Lugiso mfanyabiashara wa Kariakoo
“Huduma hii imewasaidia wananchi wengi ambao mara nyingi hushindwa kupima afya kutokana na gharama.Tunashukuru kwa huduma hii ya bure. Inawasaidia wengi wetu ambao hatukuwa na uwezo wa kugharamia vipimo”, alisema Mohamed Issa mkazi wa Ilala.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupima afya ya moyo pamoja na watoto wangu ambao nimekuja nao, huduma ni nzuri na ya kuridhisha. Nawahamasisha wananchi wengine wajitokeze kupima afya zao”, alisema Zelda Joas mkazi wa Temeke.
JKCI imeendelea na jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia kampeni mbalimbali za upimaji wa afya zikiwa na lengo la kuwahamasisha watu kufahamu namba zao za afya kama njia ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, hususan magonjwa ya moyo.
