MTOTO WAKO AKIPATA CHANJO ANAJIKINGA NA MAGONJWA

 

Na Hassan Kimweri, WAF – Mwanza

Kuelekea uzinduzi wa Chanjo ya Polio nchini, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amewataka wazazi/walezi katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Mara, Tabora pamoja na Singida kuwapeleka watoto wao ili kupata chanjo kwa lengo la kuwakinga na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. 

Dkt. Magembe amesema hayo kwenye Mkutano Mkuu wa viongozi na wadau wa Sekta ya Afya uliolenga kujadilia masuala ya mipango na utekelezaji wa huduma za chanjo nchini. 

“Chanjo hizo zitatolewa nyumbani, shuleni, vituo vya tiba na maeneo mengine ya wazi, kote huko tutawafata watoto na kuwachanja, ni muhimu sana kwa sababu ziko nchi kadhaa zina mlipuko wa polio, hivyo kama wizara tumeona ni muhimu watoto wetu wakapata chanjo ,” amesema Dkt. Magembe 

Aidha, Dkt. Magembe amesema Tanzania ipo vizuri kwenye asilimia 98% za utoaji wa chanjo ikiwemo chanjo ya kujikinga na kifua kikuu, Surua na rubela pamoja na polio, kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

“Hizi asilimia mbili zilizobaki tumedhamiria lazima twende tukawatafute hao watoto wako wapi na tujue kwanini hwakuchanjwa na tuweze kuwahudumia. Mtoto mmoja tu asiye chanja kwenye jamii anaweza kuwa ni chanzo cha mlipuko na watoto wengine wakapata magonjwa,” amesema Dkt. Magembe 

Amesema, watoto walio chanjwa chanjo ya Surua na wakapata dozi zote mbili ni chini ya asilimia 10% ndio walipata ugonjwa huo, ina maana watoto zaidi ya asilimia 91% wote hawakupata ugonjwa wa Surua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Otilia Gowele amesema, mafanikio ya chanjo ndio yamekua yakiibeba Sekta ya Afya hivyo ni muhimu kusimamia afua hiyo ili kuendelea kuikinga jamii na magonjwa mbalimbali ya milipuko.     

Post a Comment

Previous Post Next Post