TRC YAWASHIKA MKONO WAATHIRIKA WA MAFURIKO IFAKARA -MOROGORO, MBUNGE ATOA WITO

 

Na Fredy Mwanjala,

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Wananchi wa kaya 150 za kata za Kibaoni, Michenga, Lumemo na Lipangalala katika Halmashauri ya mji wa Ifakara, Jimbo la Kilombero, Mkoani Morogoro, wamelishukuru Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kuwapatia msaada wa tani kumi za unga, unaolenga angalau kupunguza adha, kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha Machi 24 na 25, 2026.

Msaada huo umepokelewa na Mbunge wa jimbo la Kilombero. Mheshimiwa Abubakari Asenga, mbele ya wananchi wa kata hizo katika hafla fupi iliyofanyika kijiji cha kibaoni, kata ya kibaoni, Halmashauri ya mji wa Ifakara, Mkoani Morogoro.

Akizungumzia msaada huo, Mheshimiwa Asenga, amesema analishuru Shirika la Reli Tanzania, kuwasaidia wananchi wa Ifakara walioathirika na mafuriko hayo a kutoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, mashirika kuiga mfano wa TRC.

“Shirika letu la Reli limeonesha mfano mzuri sana, hiki walichokitoa ni kikubwa sana na wananchi wa Ifakara wamepokea kwa mikono miwili, niendelee kutoa rai kwa mashirika mengine ya serikali na binafsi yajitoe tuweze kuwasaidia wananchi waliokumbwa na adha ya mafuriko” alisema Mhe.Asenga.

Katika hatua nyingine, Bi.Maua Mang’ula, mkazi wa Ifakara amesema msaada huo unaashiria mahusiano mazuri kati ya TRC na wananchi jamii ambayo ndio watumiaji na walinzi wakubwa wa huduma na miundombinu ya TRC .

Aidha, Sebastian George, mkazi wa kata ya Lipangalala, ameongeza kuwa, wananchi wa Ifakara wataendelea kutoa ushirikiano kwa TRC katika kuilinda miundombinu ya reli na kutokomeza vitendo vya uhalifu.

Awali, Mkuu wa kitengo cha Uhusiano cha TRC, Bw. Fredy Mwanjala, alisema TRC, imeguswa na hali iliyowakumba Watanzania, wa Jimbo la Kilombero kufuatia mafuriko aidha, kwa niaba ya Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa TRC na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Machibya Shiwa, TRC inatoa msaada wa tani 10 za unga zenye thamani ya shilingi milioni 16, angalau kusaidia kupunguza makali ya athari iliyojitokeza. 

 Aidha alisema, TRC inaelewa kuwa msaada huo hauondoi maumivu yote, lakini ni ishara ya mshikamano wa taasisi na wana Kilombero na kwamba iko karibu na wananchi katika nyakati zote ikiwemo nyakati hizi

Mvua iliyonyesha usiku wa Machi 24 na 25, 2026, ilisababisha pia kukatika kwa barabara kuu ya Ifakara- Mlimba katika maeneo ya Chita, Mbingu na Chage.    

Post a Comment

Previous Post Next Post