Wafanyabiashara marufuku kupandisha mafuta

 

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia James Mataragio leo amefanya ziara ya ukaguzi katika maghala ya kuhifadhi mafuta yaliyopo Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Mataragio amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wafanyabiashara watakaobainika kuficha mafuta kwa lengo la kuyauza kwa bei ya juu.

Ameeleza kuwa Serikali imepokea malalamiko kuhusu ucheleweshaji wa makusudi katika upakiaji wa mafuta pamoja na baadhi ya vituo kukosa huduma hiyo, hali iliyochochea kufanyika kwa ukaguzi huo ili kubaini ukweli wa mambo. “Serikali inataka kuhakikisha mafuta yanapatikana na yanafika katika vituo vyote nchini,” alisema Dk. Mataragio.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James  Andilile amesema changamoto za upatikanaji wa mafuta katika soko la dunia zimechangiwa na athari za migogoro ya kimataifa, ikiwemo vita vinavyoendelea katika baadhi ya maeneo.

Hata hivyo amesisitiza kuwa Serikali ilichukua hatua mapema kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika na kwamba kwa sasa hakuna uhaba wa mafuta nchini. Ziara hiyo imelenga kujiridhisha na hali ya upatikanaji, uhifadhi na usambazaji wa mafuta, pamoja na kufuatilia taarifa za kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya maeneo nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post