Mwandishi Wetu Morogoro,
Watumishi wa idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wamekutana mjini Mororgoro kuweka mikakati ya kuongeza ubunifu na ufanisi katika kutoa elimu ya kodi, huduma bora kwa mteja na kufanya mawasiliano ya kimkakati yenye lengo la kuongeza uelewa na kurahisisha ulipaji kodi kwa hiari.
Akifungua kikao kazi hicho, Mwenyekiti ambaye ni Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja Bw.Hudson Kamoga, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara hiyo Bw. Richard Kayombo, amewataka watumishi hao kuongeza ubunifu na kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu mkubwa na weledi huku akiwakumbusha kuwa wana jukumu muhimu la kuhakikisha wanawahudumia walipakodi kwa kuzingatia misingi ya huduma kwa wateja ili kulinda taswira ya TRA na taifa kwa ujumla.
“Tunalo jukumu muhimu la kuhakikisha tunawahudumia walipakodi kwa kuzingatia misingi ya huduma kwa wateja, kuendelea kulinda taswira ya mamlaka pamoja na kuwa wabunifu katika kufanya mawasiliano ya kimakati yanayolenga kuongeza uhiari wa ulipaji kodi” amesema Bw. Kamoga.
Aidha, amewataka maafisa hao kuwa makini wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa kuhakikisha kila mmoja anatumia taaluma yake katika kuifanya TRA kuendela kuwa taasisi inayoaminiwa na watanzania na inayowatumikia walipakodi kwa weledi wa hali ya juu.
Akihitimisha hotuba yake amewaasa maafisa wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kuendela kufanya kazi kwa kushirikiana kwani TRA inawaamini na kwa pamoja wanaweza kuwahudumia watanzania kwa uaminifu na kuleta matokeo chanya katika ukusanyaji wa kodi nchini.
Naye Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi TRA Bw. Paul Walalaze, ametoa wito kwa maafisa hao kuendelea kuuelimisha umma kuhusu faida za mifumo ya kikodi iliyopo sambamba na kuwataka maafisa hao kuwa mstari wa mbele katika kuuelimisha umma juu ya madhara ya ukwepaji kodi hasa magendo, kwani yanarudisha nyuma maendeleo ya Taifa na kuathiri afya za watanzania.
Kikao kazi hicho cha Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kinafanyika kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 12-14 Februari, 2026 na kujumuisha maafisa wa Idara kutoka Makao Makuu na Ofisi mbalimbali za TRA nchi nzima pamoja na baadhi ya wastaafu wa TRA ambao walikuwa wakifanya kazi katika idara hiyo.


.jpg)


