Mwandishi Wetu,
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amewataka watendaji wa Sekta ya Maji nchini kutumia mifumo ya kiteknolojia kubaini na kudhibiti changamoto ya upotevu wa maji pamoja na kusimamia viwango na ubora wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa miradi ya maji, ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Ametoa maelekezo hayo Februari 11, 2026 mkoani Manyara akizindua Mpango wa Gharama za Uwekezaji wa Huduma za Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (WASH), unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 94.62 kwa miaka mitano.
Amesema mpango huo umeainisha hali ya sasa, mahitaji yaliyopo, malengo yanayotarajiwa kufikiwa pamoja na rasilimali zitakazohitajika kuhakikisha wananchi wa Hanang' wanapata huduma bora ya maji safi, vyoo bora na mazingira salama.
Amesisitiza ili kuboresha huduma ya maji na kupunguza malalamiko ya wateja kuhusu ankara, mamlaka za maji na vyombo vya watumia maji vinapaswa kuongeza kasi ya ufungaji wa Dira za maji za malipo ya kabla na kuimarisha ufanisi katika utendaji kazi ili kudhibiti upotevu wa maji ikiwemo mivujo.
Amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa Gridi ya Maji ya Taifa unaolenga kuunganisha na kuimarisha mifumo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa maji nchini, hatua itakayoongeza uhakika wa upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Ameongeza Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi, imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji katika maeneo ya mijini na vijijini.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa sekta hiyo kushirikiana na wadau pamoja na wananchi kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho, na kupongeza shirika la WaterAid Tanzania kwa kuratibu maandalizi ya mpango huo.







.jpg)


