Bodi ya STAMICO yaahidi neema mgodi wa STAMIGOLD

 

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Balozi Simon Sirro amesema bodi inafuatilia na kutatua changamoto za Mgodi wa STAMIGOLD ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.

Balozi Sirro ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua maendeleo ya mgodi wa STAMIGOLD uliopo wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na kisha kuzungumza na watumishi wa mgodi huo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magala.

Amesema bodi imejipanga kusimamia kikamirifu mgodi huo unaomilikiwa na STAMICO kwa asilimia 99 ambapo itaendelea kuongeza raslimali watu na kuboresha miundombinu ya mgodi.

Amekiri kuridhishwa na usimamizi thabiti wa STAMICO katika mgodi wa STAMIGOLD ambao umeendelea kupiga hatua kubwa kila mwaka tangu ulipomilikiwa na serikali mwaka 2013 kutoka kwa mwekezaji wa kigeni.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa STAMIGOLD, Ali Said.

Aidha Sirro ameagiza STAMIGOLD kuendelea kujikita kwenye tafiti ili kubaini maeneo yanayofaa kwa uchimbaji ili kupanua uwigo wa uwekezaji na kufikia malengo ya kuongeza mapato.

Sirro ametumia nafasi hiyo pia kusisitiza nidhamu katika matumizi ya fedha za umma kwa watendaji walioaminiwa na kupewa nafasi mbalimbali za kusimamia na kuendesha mgodi huo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magala amesema STAMIGOLD tayari imeanza miradi mipya kwenye maeneo matatu ya uchimbaji yanayotarajiwa kuongeza uzalishaji.

Mgodi wa STAMIGOLD uliopo. Wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

“Kwa miezi minne ijayo, hadi kufikia Juni 2026 tunatarajia kuzalisha wakia za dhahabu 8,000, tunaamini kwamba kupitia hii itasaidia mgodi wetu wa STAMIGOLD kupiga hatua”, amesema.

Amesema pia STAMIGOLD imejipanga kufanya tafiti kwenye leseni ambazo hazijawahi kuguswa ili kuongeza uhai wa mgodi huo kutoka miaka mitano ijayo na kufikia zaidi ya miaka 10.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa STAMIGOLD, Ali Said amesema mpaka sasa mgodi umajiri wafanyakazi 613 ambao wanapambana kutimiza wajibu wao ili kuongeza mapato ya mgodi.

Amesema tangu mwaka 2013, STAMIGOLD imechangia sh bilioni 56 serikalini na juhudi zinaendelea kuhakikisha uwekezaji uliofanyika unasaidia watanzania kupata manufaa ya mgodi.

Ali ameihakikishia bodi ya Wakurugenzi ya Stamico kuwa utatuzi wa changamoto zilizopo utachochea kiwango cha uzalishaji kutoka wastani wa kilo 30 dhahabu kwa mwezi.

Post a Comment

Previous Post Next Post