MENEJIMENTI YA TRA YAKUTANA NA WASHINDI WALIOTOA MAWAZO YA UBUNIFU


 Mwandishi Wetu,

Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambayo ndio kamati ya uongozi wa juu wa shughuli za kiubunifu chini ya Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda imefanya kikao cha kusikiliza na kujadili mawazo ya wabunifu 9 waliotoa mawazo ya kiubunifu katika kuimarisha na kuongeza mapato.

Wabunifu hao wamefanya mawasilisho ya mawazo yao kwa menejimenti ya TRA tarehe 12.02.2026 katika ukumbi wa mikutano wa TRA jijini Dar es Salaam. 

Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda amewapongeza washiriki wote waliotoa mawazo ya kibunifu huku akisema kuwa TRA ilipokea mawazo mengi kutoka kwa wadau mbalimbali jambo ambalo limeonesha uzalendo wa hali ya juu kwa watanzania kukaa na kuwaza namna bora ya kuboresha usimamizi wa kodi na kuongeza mapato kwa maendeleo ya Taifa.

“Tulipokea mawazo mengi kutoka kwa watanzania na hii inadhihirisha uzalendo wa hali ya juu wa kuboresha usimamizi wa kodi na kuongeza mapato kwa maendeleo ya Taifa” Amesema Bw. Mwenda.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango ambaye ndiye anayesimamia kitengo cha Utafiti na Ubunifu Bw. George Hellar, amesema jumla ya mawazo 5602  yalipokelewa kutoka kwa wadau wa nje ya TRA na mawazo 106 yalipokelewa kutoka kwa watumishi wa TRA ambapo yamepitia kamati ya ufundi na kufanyiwa tathmini na mchujo.

Kati ya mawazo yaliofanyiwa tathmini na mchujo ni mawazo 9 yaliyoweza kukidhi vigezo vya kuchukuliwa na kuwasilishwa kwenye menejimenti ya TRA kwa ajili ya kuyajadili zaidi na kuona namna ya kuyatumia mawazo hayo katika kuboresha usimamizi wa kodi na kuongeza mapato kwa maendeleo ya Taifa. 

Aidha, Kamishna Mkuu Mwenda ameagiza Idara ya Utafiti na Mipango ya TRA  kushirikiana na idara mbalimbali na mikoa yoote ya kikodi kuhakikisha TRA inapata masuluhisho ya changamoto mbalimbali katika usimamizi wa kodi yenye ubunifu na kuleta tija huku akisisitiza kuwa anatamani kuona ubunifu katika kila kazi na shughuli mbambali zinazofanyika TRA katika kukusanya kodi.



Post a Comment

Previous Post Next Post