Mwandishi Wetu,
Zaidi ya wawekezaji 450 wa ndani na wa kimataifa wamekutana jijini Dar es Salaam katika Jukwaa la Uwekezaji katika Uzalishaji wa Dawa Tanzania, huku Serikali ya Tanzania ikitoa hakikisho la ulinzi madhubuti wa soko kwa wawekezaji wa viwanda vya kutengeneza dawa watakaozalisha kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vya kimataifa.
Akifungua jukwaa hilo jana, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema serikali imejipanga kikamilifu kulinda wawekezaji wa ndani na nje dhidi ya ushindani usio wa haki unaotokana na uingizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.
Jukwaa hilo, lililofanyika chini ya kaulimbiu “Kufungua Fursa za Tanzania kama Kitovu cha Kikanda cha Uzalishaji wa Dawa,” liliwakutanisha wawekezaji kutoka Tanzania pamoja na nchi mbalimbali zikiwemo Uganda, Canada, Uingereza, Ufaransa, Latvia, Pakistan, India, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Ujerumani.
Mchengerwa alisema serikali haitawavutia wawekezaji kisha kuwaacha wakikabiliwa na ushindani usio wa haki.
“Tanzania haiwaiti muwekeze halafu iwaache bila ulinzi,” alisema.
Alifafanua kuwa wawekezaji watakaokidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO), viwango vya Good Manufacturing Practice (GMP) na kuzalisha dawa kikamilifu nchini, watapatiwa ulinzi wa moja kwa moja wa serikali, ikiwemo uhakika wa soko kupitia manunuzi ya umma na upendeleo kwa dawa zinazozalishwa ndani ya nchi.
Aidha, alisema serikali itatumia nyenzo za kifedha na kisheria kudhibiti ushindani usio wa haki, ikiwemo hatua kali dhidi ya dawa hafifu na vitendo vya kumwaga bidhaa sokoni (dumping).
“Hakuna mwekezaji atakayejenga kiwanda Tanzania halafu akavunjwa moyo na uingizaji holela wa dawa kutoka nje. Enzi hizo zimekwisha,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha dawa zinazozalishwa nchini zinakubalika katika soko la ndani, kikanda na kimataifa, huku Tanzania ikijijenga kama kitovu cha kuaminika cha uzalishaji wa dawa barani Afrika.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Munde, alisema sekta ya uzalishaji wa dawa inanufaika na motisha mbalimbali ikiwemo misamaha ya kodi kwa mitambo na malighafi, pamoja na upatikanaji wa ardhi katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ), hatua inayopunguza gharama za uendeshaji na kutoa uhakika wa soko.
Mwenyekiti wa Chama cha Watengenezaji wa Dawa Tanzania (TPMA), Bashiru Haroun, alisema utulivu wa kisiasa na kiuchumi wa Tanzania unaifanya nchi kuwa kivutio salama kwa uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya dawa.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, alisema jukwaa hilo limekuwa fursa muhimu ya kuunganisha wawekezaji wa ndani na wa kimataifa, kuonesha ukuaji wa soko la Tanzania na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

