WAGONJWA 760 KUNUFAIKA NA MPANGO WA BILIONI 6.7 WA SERIKALI

 

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) akiwa katika picha ya pamoja na wakurugenzi wa Taasisi za Afya mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi na watumishi wa sekta hiyo kilichofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) akizungumza na wafanyakazi wa sekta ya afya wakati wa kikao kazi na watumishi hao kilichofanyika wiki hii katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliyopo jijini Dar es Salaa.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa ziara yake ya kazi na kuzungumza na watumishi wa sekta ya afya aliyoifanya wiki hii katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) wakati wa kikao kazi na watumishi wa sekta ya afya kilichofanyika wiki hii katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Serikali ya awamu ya sita imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.7 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwaajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma za ubingwa bobezi kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo.

Fedha hizo zimelenga kuwahudumia wagonjwa takribani 760 wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa na Taasisi zinazotoa huduma za ubingwa bobezi ikiwemo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza hivi karibuni na wafanyakazi wa sekta walioko mkoa wa Dar es Salaam Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema hatua hiyo ni muendelezo wa yaliyofanyika mwaka 2024/2025 ambapo serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni nane zizizogharamia matibabu ya wagonjwa 677 wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya kibingwa.

Aidha Mhe. Mchengerwa alizitaka hospitali zote nchini kuboresha ubora wa huduma na kuanza mchakato wa kupata ithibati za kimataifa zitakazowawezesha kutambulika kimataifa na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia katika kutoa huduma bora za afya.

Mhe. Mchengerwa alisema hospitali hizo zinatakiwa kuhakikisha zinatoa huduma bora salama na zenye kuwajali wagonjwa ili ziweze kupata ithibati itakayowasaidia kubeba soko la kimataifa, kutambuliwa kimataifa na kuongeza pato la taifa.

“Naipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuanza mchakato wa kupata ithibati za kimataifa (ISO) katika kutoa huduma za ubingwa bobezi za magonjwa ya moyo nchini na nimesikia ipo katika hatua nzuri, hongereni sana”, alisema Mhe. Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa alizitaka hospitali hizo bingwa kuimarisha huduma za upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa, kuimarisha afya na kinga zaidi kuliko tiba, kuimarisha utafiti, ubunifu na tiba shirikishi na kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kutoa huduma.

“Kwa nini mgonjwa azunguke vitengo mbalimbali vya hospitali kufungua faili wakati teknolojia inaruhusu kufungua faili hilo mtandaoni. Ninawaomba kupitia TEHAMA anzisheni mfumo wa One Stop Digital Center mara moja ambao mgonjwa anaweza kufungua faili lake akiwa mtandaoni, akapata control namba ya malipo ya huduma akiwa mtandaoni, hii itapunguza foleni na muda wa kukaa hospitali”, alisema Mhe. Mchengerwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mambo mengi yaliyosemwa na Mhe. Waziri katika hotuba yake JKCI imeshayafanyia kazi ikiwemo hatua za kupata ithibati za kimataifa, mambo ya kuendesha taasisi kimtandao na masuala mbalimbali ya wafanyakazi.

“Tumefurahi leo kukutana na Mhe. Waziri wa afya kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe, tunashukuru kwa maelekezo yake na tunaahidi kuwa JKCI tutayatekeleza yale yote aliyoyasema”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema JKCI inaahidi kuendelea kuwahudumia vizuri wagonjwa wake na kuyafuata yote aliyoyaelekeza Mhe. Waziri wakiwa na lengo la kufikisha huduma bora kwa wananchi na kufuta kabisa haja ya wagonjwa kwenda nje ya nchi kupata huduma za ubingwa bobezi za moyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post