NA MWANDISHI WETU
MGOMBEA Udiwani Kata ya Kinyerezi katika Jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Ryoba 'Wahenga' amesema kwamba ikiwa atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo moja ya mikakati yake ni kuishauri Serikali kuunda chombo kitakachosimamia Barabara za Mitaa.
Ryoba, akizungumza jana Agosti 31, 2025 na Mwandishi Wetu, Kinyerezi wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, alitanabaisha kuwa kumekuwepo na changamoto kubwa ya kuzifanyia ukarabati barabara za mitaa chini ya Wakala wa Barabara za Vijijni na Mijini (TARURA), hivyo kukiwa na chombo mbadala itasaidia kuleta ufanisi unaohitajika.
“Nikifanikiwa kupata ridhaa ya wananchi ya kuwa diwani wa kata hii, nitaishauri Serikali kupitia vikao vya Baraza la Madiwani iunde chombo kitakachosimamia Barabara za Mitaa na Tarura iachwe ishughulike na barabara za vijijini pekee ili kuleta uangalizi wa karibu na wenye ufanisi unaohitajika,” amesema.
Aidha amesema kuwa kutokana na yeye kuwa mjasiriamali kuingia kwake kwenye siasa atatumia fursa hiyo kukutana na wawekezaji walio katika kata hiyo, hususan wamiliki wa vituo vya mafuta walio pembezoni mwa barabra ya Kirenyezi ili watoe ajira kwa wakazi kata hiyo.
Amefafanua kwamba kutokana na uwekezaji wa baadhi ya vituo hivyo kuwepo katika kata hiyo pembezoni mwa barabaya Kinyerezi ni vema wakazi wa maeneo hayo wakawa ni miongoni mwa wanafuika wa ajira hizo.
Pia amesema katika mradi unaendelea wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II, nako atashawishi viongozi ili baadhi ya wafanyakazi watoke katika hiyo na si kuwa watazamaji wa miradi inayofanyika bila ya kunufaika kwa njia moja au nyingjne.
Mteule huyo kupitia CCM kuwania nafasi ya udiwani katika kata hiyo, pia amebainisha kuwa ikiwa atafanikiwa kuwa diwani atashughulikia migororo yote ya ardhi ambayo tayari baadhi yake anaifahamu vema ukiwemo uliopo eneo la Kamzora Kifuru.
Aidha amejipanga ikiwa atakuwa diwani wa kata hiyo kusimamia vema ujenzi wa Zahanati katika eneo la Kifuru ambao umekwama kwa kipindi kirefu na kuleta adha kwa wakazi wa eneo hilo kutafuta huduma ya afya kupitia kituo cha Serikali.