TFRA YAWATAKA WAFANYABIASHARA KUUZA MBOLEA ZILIZOSAJILIWA NA MAMLAKA


 Wafanyabiashara wa mbolea nchini wametakiwa kuhakikisha wanauza na kusambaza mbolea zilizosajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili kuepuka uvunjifu wa  Sheria ya Mbolea na kujingiza katika makosa yatakayopelekea kufungiwa leseni ya kufanya biashara hiyo.

Hayo yameelezwa na Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Raymond Konga, wakati wa mafunzo ya mbolea kwa wasambazaji na  wafanyabiashara wa mbolea wa Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Agosti 2025.

Konga ameongeza kuwa, mfanyabiashara yeyote anayebainika kukiuka sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara hiyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kulipa faini au kufikishwa mahakamani.

Aidha, katika mafunzo hayo, wafanyabiashara wameelezwa hatua za kuzifuata ili waweze kusajiliwa na kupata leseni ya kufanya biashara ya mbolea pamoja na masuala mengine ikiwa ni pamoja na hatua za usajili wa mbolea mpya. 

Kwa upande wao, wafanyabiashara walioshiriki waliishukuru TFRA kwa mafunzo hayo na kuahidi kuzingatia sheria, taratibu na miongozo yote kama walivyoelekezwa ili kuimarisha biashara zao na kuunga mkono jitihada za serikali katika kudhibiti ubora wa mbolea nchini.



Post a Comment

Previous Post Next Post