TFRA YAWAKARIBISHA WANANCHI WA MOROGORO NA LINDI KWENYE MAONESHO YA NANENANE 2025

 Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inawakaribisha wananchi wote kutembelea mabanda yake katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Julius K. Nyerere mkoani Morogoro na Ngongo mkoani Lindi yaliyoanza tarehe 1 na kuhitimishwa tarehe 8 Agosti 2025.

Meneja wa TFRA, Kanda ya Mashariki, Daniel Maarifa, amesema kuwa mwaka huu banda la TFRA limepanua wigo wa utoaji elimu kwa kujumuisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya mbolea, sambamba na elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.

Ameeleza kuwa, teknolojia hizo ni pamoja na vifaa vya kupima afya ya udongo, matumizi ya mbolea za kisasa zinazoingia haraka kwenye mmea, na mbinu za kupulizia mbolea kwa kutumia maji ili kuongeza kasi ya ufanisi kwenye uzalishaji.

Maarifa amebainisha kuwa, kupitia mabanda haya, wananchi watapata fursa ya kuelewa kwa undani namna mbolea zinavyopimwa ubora wake kuanzia zinapowasili nchini, hatua za ukaguzi bandarini, uchukuaji wa sampuli hadi vipimo vya kimaabara vinavyofanywa kabla ya mbolea kufika sokoni.

Amesema ili mkulima aweze kusajiliwa kwenye mfumo rasmi wa pembejeo za ruzuku anatakiwa kuwa na kitambulisho cha NIDA au cha mpiga kura, namba ya simu na taarifa za eneo la shamba lake ikiwa ni kijiji na ukubwa wa shamba analolima.

TFRA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kuhakikisha kuwa wakulima wanapata taarifa sahihi na huduma bora zitakazowawezesha kuongeza tija katika kilimo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Wananchi wa Morogoro na Lindi mnahimizwa kujitokeza kwa wingi kutembelea mabanda ya TFRA ili kunufaika na elimu, huduma na teknolojia zitakazowasaidia kubadilisha kilimo chenu kuwa cha kisasa na chenye tija zaidi.





Post a Comment

Previous Post Next Post