TFRA Yajizolea Tuzo Tatu Katika Maonesho ya Nane Nane 2025

 Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imepata mafanikio makubwa katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane 2025 baada ya kujinyakulia jumla ya tuzo tatu katika kanda mbalimbali nchini. Mafanikio haya ni kielelezo cha jitihada endelevu za TFRA katika kusimamia ubora wa mbolea na kutoa elimu kwa wakulima nchini.

Katika maonesho yaliyofanyika mkoani Mbeya, TFRA iliibuka mshindi wa pili, ikiwa ni matokeo ya maandalizi bora na elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na kanuni bora za kilimo. Banda la TFRA lilivutia mamia ya wakulima waliopata fursa ya kujifunza mbinu za kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji wa mazao.

Aidha, katika Maonesho ya Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika mkoani Arusha, TFRA pia ilishinda nafasi ya pili. Ushindi huu ulitokana na ubunifu wa mabanda, utoaji wa huduma rafiki kwa wakulima, pamoja na mbinu shirikishi za elimu kupitia mafunzo ya vitendo na mashamba ya mfano.

Kanda ya Ziwa Mashariki nayo haikubaki nyuma, ambapo TFRA ilishinda nafasi ya tatu katika maonesho yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Nyakabindi, mkoani Simiyu. Timu ya watumishi wa TFRA ilitoa mafunzo kwa wadau wa kilimo, kuonesha matumizi sahihi  ya mbolea, na kusajili wakulima katika mfumo wa kidijitali wa pembejeo za ruzuku, jambo lililopongezwa na wageni waliotembelea banda hilo.

Tuzo hizi zinathibitisha mchango mkubwa wa TFRA katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kwa tija na ushindani. Kupitia mashamba ya mfano, elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, na usajili wa wakulima kwenye mfumo wa kidigitali  wa pembejeo za ruzuku , TFRA inaendeleza dhamira yake ya kulinda maslahi ya wakulima na kukuza uchumi wa kilimo nchini.



Post a Comment

Previous Post Next Post