Mwandishi Wetu,
Taasisi ya NAFAKA Kilimo kupitia mradi wake wa Farm to Market Alliance (FtMA) imepongeza kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na huduma nyingine za kuendeleza kilimo chenye tija. Hayo yalisemwa na mwakilishi wa taasisi hiyo, Datius Kaigwa, walipotembelea banda la TFRA katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane kwenye Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Kaigwa alieleza kuwa NAFAKA Kilimo inatekeleza mradi huo katika wilaya nane zikiwemo Mbarali, Wanging’ombe, Mufindi, Iringa DC na Kilolo, ambapo wamejipanga kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa gharama nafuu. Alisema ushirikiano na TFRA ni muhimu ili kuhakikisha elimu inayotolewa kuhusu mbolea na afya ya udongo inafika hadi ngazi ya kijiji.
Akibainisha mkakati wa utekelezaji, Kaigwa alisema taasisi hiyo inashirikiana na wasambazaji wa pembejeo, viongozi wa vikundi vya wakulima, na wakulima viongozi ili kuhakikisha taarifa na elimu ya kilimo bora zinafika kwa walengwa. Alisisitiza kuwa uhusiano wa karibu kati ya wadau hawa na TFRA utarahisisha zaidi upatikanaji wa pembejeo na kuongeza mwamko wa wakulima kutumia mbinu bora za kilimo.
Mbali na usambazaji wa pembejeo, mradi wa Farm to Market Alliance pia unatoa mafunzo ya kilimo cha kisasa na kusaidia wakulima kupata taarifa za masoko, hatua inayolenga kuhakikisha mazao yao yanauzwa kwa bei nzuri na kuwapatia kipato bora. Kaigwa alisema huduma hizi zikichanganywa na juhudi za TFRA zitasaidia sana kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mavuno.
Alihitimisha kwa kuipongeza TFRA kwa kuanzisha na kuendeleza programu za elimu kwa wakulima kupitia banda la maonesho, akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za maendeleo ya kilimo na mamlaka za udhibiti kama TFRA ndiyo njia bora ya kufanikisha malengo ya taifa ya kujitosheleza kwa chakula na kuinua uchumi wa wakulima.