
AFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Alban Kihulla, ametembelea Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni, jijini Dodoma, na kutoa pongezi kwa watumishi wa Wakala kwa kazi nzuri ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya vipimo.
Akiwa katika Banda la WMA, Bw. Kihulla amepongeza juhudi za watumishi wa taasisi hiyo kwa kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, tangu kuanza kwa Maonesho hayo.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya ya kutoa elimu ya vipimo. Ni muhimu jamii ikaelewa namna Serikali kupitia WMA inavyowalinda kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika kwenye sekta mbalimbali ni sahihi na vinatumika kwa usahihi,” amesema Bw. Kihulla.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utoaji wa elimu hiyo hata baada ya Maonesho hayo ya NaneNane ili kuendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo yao ya kazi na shughuli za uzalishaji.
“Tuendelee kutumia majukwaa mbalimbali kutoa elimu ya vipimo kwa wananchi ili waelewe haki yao ya kupata huduma kwa vipimo sahihi, lakini pia wajibu wao wa kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi katika sekta mbalimbali,” ameongeza
Mbali na kutembelea Banda la WMA, Bw. Kihulla pia amefanya ziara katika mabanda mengine mbalimbali, yakiwemo ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zilizo chini yake, kwa lengo la kujionea huduma na teknolojia zinazotolewa kwa wananchi.