MASAUNI AKOSHWA NA USIMAMIZI MIRADI YA MABADILIKO YA TABIANCHI

 

Na Mwandishi Wetu – Magu, Mwanza

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesema Tanzania ina kila sababu ya kijipongeza kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anazofanya ili Taifa kunufaika na mifuko ya Miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Masauni ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kukagua miradi iliyoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wilayani Magu mkoani Mwanza, Agosti 21, 2025 ambapo amesema wananchi wanapaswa kuilinda miradi hiyo ili kuwanufaisha zaidi.

“Tunafahamu nchi yetu inaathirika na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaathiri sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya kilimo, mifugo, maji na nyinginezo hivyo tunapaswa kuangalia namna ambavyo tutaweza kupambana katika hali hiyo,” amesema Masauni.

“Hapa Magu fursa hizo imegusa sekta ya mifugo, vikundi vya wamama na miradi ya maji na mingine, tunamshukuru Mhe. Rais kutokana na jitihada za mahusiano za nchi yetu na Jumuiya za kimataifa inavyoweza kufanya Taifa letu kufaidika na fursa hizo, kwani miradi hii imebadilisha maisha ya wananchi,” amesema Mhe. Masauni.

Pia ameupongeza uongozi wa mkoa, wilaya na wizara kwa kusimamia na kufanya wananchi kunufaika zaidi na kwa kuendesha kilimo hata kipindi cha kiangaza kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Jubileta Win Lauwo amesema amefurahishwa na ujio wa Waziri Masauni kwa kukagua miradi hiyo ambayo imegharimu fedha nyingi kwani hii inaongeza vipato kwa wananchi wa wilaya hiyo waliokuwa kwenye vikundi.

“Umekuja kukagua miradi ambayo imegharimu fedha nyingi ambazo tumepatiwa na Mh Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuwezesha wananchi wilayani hap ana sasa kila mmoja ambaye amejinga kwenye kikundi amekuwa akinufaika kwa namna moja au nyingine na kuongeza kipato chake.”

“Wananchi wa Magu na mimi kiongozi wao nipende kutoa rai ya kutosita kuleta miradi mingine kwani Wananchi wamenufaika na wengine wanakuja ofisini kwangu nao kutaka kunufaika kama wenzao, hivyo bado tunauhitaji wa miradi kama hii.”

Naye Afisa kilimo wa Kata ya Ng’aya wilayani Magu Bw. Mtatiro Jorwa amesema mradi huo una manufaa makubwa kwa sababu umeongeza uzalishaji katika kilimo sababu wakulima walikuwa wanazalisha gunia 10 kwa heka moja lakini kwa sasa wanazalisha gunia 24 baada ya kupata elimu juu ya kilimo cha kisasa.   

Post a Comment

Previous Post Next Post