Mwandishi Wetu,
Wakulima wadogo zaidi ya 550,000 nchini Tanzania watanufaika na upatikanaji wa mbolea kupitia mradi mpya wa Dhamana ya Mikopo ya Biashara kwa Sehemu (Partial Trade Credit Guarantee – PCG), baada ya dola milioni 2 za Kimarekani kutengwa kwa ajili ya kuwawezesha wauzaji wa pembejeo kupata mbolea kwa mkopo.
Mradi huo umezinduliwa rasmi tarehe 7 Agosti, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao, Usalama wa Chakula na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi, katika viwanja vya Maonesho ya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Dkt. Nindi, amesema, serikali imejidhatiti kuhakikisha wakulima walioko pembezoni wanawezeshwa kwa kupata pembejeo bora kupitia mifumo rafiki ya kifedha inayohusisha sekta binafsi.
Amesema, mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Mfuko wa Ufadhili wa Mbolea Afrika (AFFM), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), na mshirika mtekelezaji African Fertilizer and Agribusiness Partnership (AFAP), kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mbolea bora na kwa wakati kwa wakulima wadogo nchini.
“Mradi huu utatekelezwa kupitia sekta binafsi ambapo mawakala wa mbolea watawezeshwa kupata mbolea kwa mkopo, huku wakitoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima,” alisema Dkt. Nindi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema, mradi huo ni mwendelezo wa mafanikio yaliyopatikana kati ya mwaka 2019 hadi 2022 katika awamu ya awali ya utoaji wa dhamana za mikopo ya mbolea. Amesisitiza kuwa awamu hii inalenga zaidi kuwezesha wakulima wadogo kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
“Awamu hii inalenga si tu kupunguza hatari katika sekta ya kilimo, bali pia kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi, na muhimu zaidi kuwawezesha wakulima wadogo ambao ndio uti wa mgongo wa uzalishaji wa chakula nchini,” amesema Joel.
Naye Marie Claire Kalihangabo, Mratibu wa Mradi kutoka AFFM, amesema cha dola milioni 2 za kimarekani kimetengwa kama dhamana itakayowasaidia wauzaji wa kati na wadogo kupata mbolea kwa mkopo kutoka kwa wasambazaji wakubwa, huku AFFM wakigawana hatari (risk) ya kifedha itakayotokana na mikopo hiyo.