Mwandishi Wetu,
Wananchi mbalimbali wameendelea kutembelea Banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea na kueleza kuridhishwa na elimu inayotolewa na wataalam wa Mamlaka bandani hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo tarehe 3 Julai, 2025, katika viwanja vya Mwalimu Nyerere yanakofanyika maonesho hayo, baadhi ya wakulima wamesema kuwa elimu wanayoipata kupitia Banda hilo ina manufaa makubwa katika kuwawezesha kuboresha kilimo na hivyo kuongeza tija na kukuza uchumi wao.
George Masanga, mkulima kutoka mkoani Ruvuma, amesema, amefurahishwa na huduma ya usajili wa wakulima kwenye mfumo wa Kidijitali wa Pembejeo za Ruzuku na kueleza kutokana na mazingira yake kuwa magumu hakupata nafasi ya kujisajili lakini baada ya kusikia TFRA watatoa huduma hiyo wakati wa maonesho naye amekuwa mnufaika miongoni mwa wengi watakaohudumiwa.
“Huduma hii itanisaidia sana katika msimu ujao wa kilimo. Nitakuwa na uwezo wa kupata mbolea za ruzuku kwa urahisi na kwa wakati. Pia nimepata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ambayo naamini itanisaidia kuongeza uzalishaji,” amesema Masanga.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuanzisha mfumo huo wa kidijitali ambao amesema ni chachu ya maendeleo ya kilimo bora na endelevu nchini.
Kwa upande wake, Hassan Mambo, mkulima kutoka Dar es Salaam, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la TFRA ili kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kujifunza kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia sekta ya mbolea.
“Watu wengi bado hawajui kuwa mbolea hizi zinapimwa na kuthibitishwa ubora wake kabla ya kuingia sokoni. TFRA inatoa elimu ya msingi kuhusu hilo, na ni muhimu kwa wakulima wote kuifahamu,” amesisitiza Mambo.
Naye Daudi Sanga, mkulima kutoka mkoani Njombe, ameishauri Serikali kuendelea kusogeza karibu huduma zinazowagusa wakulima moja kwa moja ili kuwawezesha kulima kwa tija kwa kutumia mbinu za kisasa.