Wakulima wa pamba Igunga wanufaika na elimu ya Matumizi sahihi ya mbolea

Mwandishi Wetu,

Wakulima wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wameanza kunufaika kwa kiasi kikubwa na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la pamba, elimu iliyotolewa kwa ushirikiano baina ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).

Wakizungumza wakati wa kufanya tathmini ya uzalishaji baada ya kutumia mbolea, wakulima hao wamesema wanatarajia kuvuna zaidi ya mara tatu ya walichokuwa wakivuna kabla ya kutumia mbolea.

Aidha, wakulima hao wamesema, baada kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ambayo iliambatana na ushauri wa kupima afya ya udongo wamechukua hatua za makusudi kwa kupima na kutambua aina na kiasi cha virutubisho kinachohitajika kwenye mashamba yao na hivyo kutumia mbolea kwa usahihi.

Kufuatia manufaa waliyoyaona msimu huu, wakulima wa pamba wameahidi kuendelea kutumia mbolea kwenye kilimo ili kuendelea kunufaika na tija inayotokana na matumizi sahihi ya mbolea. 

Akishuhudia hayo mkulima, Lucas Sita aliyetenga nusu ya shamba lake na kutumia mbolea na nusu kapanda bila mbolea anaeleza kuwa, shamba alilotumia mbolea limestawi vizuri na kuwavutia wakulima wenzake ambao hawakusita kumtembelea ili kujifunza mbinu alizotumia na kupelekea kuongeza uzalishaji.

Lucas anaeleza kuwa, kabla ya kutumia mbolea kwenye kilimo chake alikuwa akivuna kilo 200 kwa ekari, lakini msimu huu anatarajia kuvuna zaidi ya kilo 1,700 kutokana na tathmini iliyofanywa na wataalamu.

"Kwa kweli nimeonja faida ya kutumia mbolea, siwezi kuacha kuitumia" Lucas alisisitiza.

Naye, Afisa Ugani wa kijiji cha  Mwabakima Kata Mbutu wilayani Igunga, Regan Kimario amesema, wakulima wa Kata hiyo wamenufaika na elimu ya mbolea na kilimo cha kuzingatia kanuni bora za kilimo ambayo imeongeza uzalishaji kutoka chini ya kg 500 hadi kufikia zaidi ya kilo 1,000 za pamba kutegemeana na  namna mkulima anavyohudumia shamba lake na hali ya hewa.



Post a Comment

Previous Post Next Post