Mwandishi Wetu,
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kuimarisha mshikamano na ushirikiano baina yao ili kufanikisha malengo katika kurekebu/kudhibiti na kuimarisha tasnia ya mbolea nchini.
Mkurugenzi Laurent ametoa wito huo wakati wa kikao kazi baina yake na watumishi wa Mamlaka kilichofanyika tarehe 7 Mei, 2025 katika Ukumbi wa Maabara ya Mbolea ya TFRA Vetenari jijini Dar es Salaam.
Laurent amesema kwa kiasi kikubwa anaridhishwa na utendaji wa watumishi wa TFRA, jambo ambalo limepelekea kupungua kwa malalamiko kutoka kwa wadau na kuboreshwa kwa huduma kwa wakulima.
Akisisitiza umuhimu wa mshikamano, Laurent alinukuu kauli mbiu yake isemayo "None of us is as good as all of us", akieleza kuwa kila mtumishi ana mchango muhimu katika kutekeleza majukumu ya Mamlaka kama ilivyokasimiwa kisheria.
Akibainisha mafanikio yaliyopatikana katika msimu wa kilimo 2022/23 na 2023/24, Bw. Laurent alisema kuwa kupitia mifumo ya Fertilizer Information System (FIS) na Mfumo wa Kidigitali wa Pembejeo za Kilimo, TFRA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufuatilia mnyororo mzima wa mbolea kutoka zinapoingia nchini hadi kwa mkulima wa mwisho.
Pia, alieleza kuwa uzalishaji wa mbolea kwa viwanda vya ndani umeongezeka kutoka tani 100,000 mwaka 2022/2023 hadi tani 232,000 mwaka 2023/2024, huku matumizi ya mbolea yakiongezeka kutoka tani 580,000 hadi 840,000 kwa kipindi hicho na mengine mengi.
Aidha, Mkurgenzi Laurent ameipongeza Idara ya Huduma za Mamlaka kwa kuandaa mafunzo ya maadili na afya mahali pa kazi na kwani yatasaidia kuimarisha utendaji na kuwawezesha watumishi kuepuka changamoto za kiafya zinazosababishwa na mazingira ya kazini na kifamilia.
Mwisho, Laurent amewasihi watumishi kutumia changamoto wanazokutana nazo kama fursa ya kujifunza na kuboresha utendaji wakizingatia kasi ya mabadiliko ya teknolojia ili wasiwe nyuma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mamlaka, Victoria Elangwa ameshukuru kwa hotuba nzuri yenye maelekezo yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa weledi.




