TFRA imewataka wakulima wa Kahawa kuzingatia kanuni bora na Teknolojia kwenye kilimo cha kahawa

Mwandishi Wetu,

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) amewataka wakulima wa Kahawa Mbinga Mkoani Ruvuma  kuzingatia kanuni bora za kilimo cha kahawa na mazao mengine  kwa kutumia teknolojia bora za kilimo ili waweze kuongeza tija ya uzalishaji, fursa ya kujiajiri ili kuondokana na umaskini. 

Dkt. Diallo ametoa ushauri huo tarehe 27 Mei, 2025, Mkoani Ruvuma ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Bodi ya TFRA  lengo kuu likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku katika mazao ya kimkakati ya kahawa na parachichi kwa mikoa ya nyanda za juu kusini.

Dkt. Diallo amesema kuwa,  gharama na nguvu anayotumia mkulima kuwekeza kwenye ekari moja ya shamba la kahawa, lazima ilingane na thamani ya uzalishaji unaotarajiwa ambao ili kuupata ni lazima mkulima azingatie kutumia maarifa na sayansi katika uzalishaji wa zao la kahawa.

Akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya mbinga, Kanisius Marco, Dkt. Diallo na wajumbe alioambatana nao walipata taarifa kuhusu hali ya upatikanaji na matumizi ya mbolea pamoja na uwepo wa vitendea kazi hususan mashine za kuchunguza afya ya udongo (Soil Scanner). 

Aidha, Mkuu wa Wilaya, Marco ameeleza kuridhishwa na  ushirikiano baina ya TFRA na watendaji ngazi ya Mkoa, Wilaya hadi vijiji unaowezesha kuwafikia wakulima  na kutatua changamoto zao kwa wakati.  

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo wa Mkoa wa Ruvuma,  Afisa Kilimo Onesmo Mpuya, ameishukuru Serikali kwa mpango wa ruzuku, akisema kabla ya mpango huo walikuwa wakikadiria matumizi ya mbolea bila uhakika, lakini sasa kupitia mfumo wa pembejeo, wanaweza kupata taarifa sahihi za matumizi na kufanya makadirio sahihi.

Naye Michael Kanduyu Mwenyekiti wa MBIFACU ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza mpango wa mbolea ya ruzuku iliyowezesha kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 16,000 hadi kufikia tani 24,000.



Post a Comment

Previous Post Next Post