NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt Seleman Jafo, ametoa wito kwa wasanii kusajili Alama za Biashara (logo) zinazotumika katika bendi za muziki au studio.
Jafo ametoa wito huo, leo Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kuadhimisha Siku ya Miliki Ubunifu Duniani 2025, iliyoratibiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambapo pia tuzo zilizotolewa kwa wadau ambao wamesajili kazi zao Kwa wingi.
"Alama zenu za biashara zinaweza kusajiliwa kupitia BRELA, na hivyo kupata umiliki wa kipekee utakao wawezesha kuzitumia sokoni na kuepuka logo hizo kufanyiwa uharamia,
" Pia ninawaasa wasanii kwenda COSOTA kusajili kazi zao ili kujihakikishia wanapata mirabaha ya kazi zao zinapotumika na watu wengine pasipo ridhaa ya wasanii husika.
Ameongeza kuwa jambo hilo litasaidia wasanii na wanamuziki kuwa na kipato cha uhakika na watakuwa na uwezo wa kukuza na kuboresha kazi zao.
Pia amesema kwa nafasi yake ya uwaziri mwenye dhamana na masuala ya Miliki Ubunifu, ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine kupitia BRELA na COSOTA, kuimarisha ulinzi wa haki za Miliki Ubunifu nchini.
"Ninawasihi tuungane pamoja katika kusikilizia mdundo wa miliki ubunifu" na kujenga mustakabali wa pamoja kuhakikisha wasanii na wabunifu wetu si tu wanalindwa na kuheshimiwa hapa nchini na nje ya nchi yetu, lakini pia wanapata manufaa kupitia bunifu zao.
Pia amewapongeza wote walioibuka washindi katika Tuzo za Taifa za Miliki Ubunifu (National Intellectual Property Awards (NIPA) 2025.
Amewataka tuzo ambazo wameshinda zikawe chachu ya kufanya bunifu zaidi na wahakikishe bunifu zao zinalindwa ili kuwaepusha na uharamia na kuwapatia manufaa zaidi.
Aidha amesema kwa wale ambao hawakufanikiwa kupata tuzo hizo, wahakikishe sio tu wanafanya ubunifu, bali ziwe zinazolenga katika kutatua changamoto za kijamii, na kuhakikisha zinalindwa na mwisho kuingizwa sokoni.
Jafo kwa mara nyingine aliwapongeza BRELA na COSOTA kwa kuandaa maadhimisho haya ya Siku ya Miliki Ubnifu Duniani mwaka 2025, pamoja na BRELA kuweza kutoa Tuzo za Taifa za Miliki Ubunifu zinazolenga kutambua mchango mkubwa wa Wabunifu wetu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Bunifu Duniani kwa mwaka 2025 pia amewasistiza wasanii wa muziki nchini kusajili kazi zao na kuzilinda kupitia mifumo rasmi ya miliki bunifu ili kunufaika kiuchumi na kulinda kazi zao dhidi ya wizi wa ubunifu.
Nyaisa amesema licha ya muziki wa Tanzania kuvuka mipaka ya nchi, wasanii wengi bado hawajachukua hatua ya kusajili kazi zao, jambo linalowanyima fursa ya kunufaika na kazi hizo kisheria.
“Tunasisitiza muziki si burudani tu, ni biashara. Na biashara yoyote inalindwa. Wasanii wengi wanapoteza mapato kwa sababu kazi zao hazijasajiliwa,” amesema.
Kauli mbiu ya mwaka huu kimataifa ni “Muziki na Miliki Bunifu Tanzania: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu.”
Nyaisa amesema BRELA imekuwa ikitoa elimu kwa wasanii kuhusu haki zao za ubunifu na kuwasogezea huduma ili waelewe namna bora ya kulinda kazi zao.
“Wapo wasanii wa zamani ambao nyimbo zao bado zinapigwa hadi leo lakini hawapati chochote kwa sababu hawakuzisajili. Hili ni pigo kwao na kwa familia zao,” amesema.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya teknolojia yamekuwa na pande mbili; yamefungua fursa kwa wasanii lakini pia yameongeza changamoto ya matumizi holela ya kazi za muziki bila ridhaa ya wasanii.
BRELA imesema itaendelea kushirikiana na taasisi kama COSOTA ili kuhakikisha kazi za ubunifu zinalindwa na zinakuwa chanzo thabiti cha kipato.
![]() |
.png)


.jpg)




